Na Nyandazajuublog-Makete
Kufuatia hali, Katibu Tawala wa Wilaya ya Makete, Grace Mgeni amewataka wananchi wilayani Makete kuachana na tabia za kuwatenga wanawake ili wasiweze kupata haki za kuwa na ardhi, jambo ambalo alisema linaonyesha dhahiri mwanamke bado anabaguliwa.
Wilayani Makete
"Katika wilaya yetu ya Makete kuna changamoto ya matumizi bora ya ardhi, hasa katika upandaji wa miti, wananchi wamekuwa wanapanda miti mpaka sehemu ambazo zinatumika kwa ajili ya kilimo cha chakula, mkakati wa wilaya ni kupunguza na kutoa ile miti ambayo imepandwa sehemu zisizostahili," alisema Grace.
"...na pia kwenye umiliki wa ardhi inaonekana mwanamke hajapewa kipaumbele sana kwenye umiliki wa ardhi, jamii itambue mwanamke naye ana haki ya kumiliki ardhi kama mwanaume, tusiwatenge tuwape haki yao," alisema.
Kwa upande wake, Afisa Ardhi wa wilaya ya Makete, Novatus Lyimo alisema kutokana na sheria za kikabila kuendelea kuwepo wilayani Makete, wanawake wamekuwa hawapewi mamlaka ya kumiliki ardhi hivi sasa.
"Sheria nyingi za kimila zinabana haki mwanamke kuweza kumiliki ardhi, tunajaribu kutoa elimu kila tunapopata fursa kuwa mwanamke ana haki ya kumiliki ardhi, lakini kwa Makete bado tunachangamoto ya mwanamke kumiliki ardhi," alisema Lyimo.
"Huku bado kuna sheria za kimila, kikabilia ambazo zinawabana wakina mama, utakutana na swali mtu anakuambia mwanamke akishaolewa, ataenda kupata ardhi kwa bwana yake, lakini akifika pia kule, akifa bwana anarudi kwao, sasa hakuna sehemu ambayo anapata ardhi, hivyo hapa Makete ni changamoto," alisema.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, hata kwenye mikutano inayoitishwa na maafisa ardhi kwa wananchi kujadili masuala ya migogoro ya ardhi, mwanamke amekuwa akinyimwa haki ya kuongea.
"Saa nyingine mwanamke kuongea kwenye mkutano hawezi kuongea, kwa sababu hizo ndizo zilivyo huku Makete, mwanaume ndiye anapaswa kuongea, kwa hiyo tunapowapa nafasi ya kuongea wanawake huwa wanashangilia sana," alisema Lyimo.
Akizungumzia namna Halmashauri inavyojikita kutatua migogoro ya ardhi wilayani Makete, Lyimo alisema bado migogoro katika halmashauri hiyo ipo licha ya kuendelea kuitatua wakishirikiana na MIICO.
"Kuna migogoro baina ya kijiji na kijiji kutokufahamu mipaka, kwa hiyo katika halmashauri yetu yenye vijiji 93 karibu vyote vina migogoro, lakini tunaenda awamu kwa awamu, MIICO kwa upande mmoja inatusaidia sana kwa sababu kwa upande wa halmashauri kinachotubana ni bajeti," alisema Lyimo.
Naye Mratibu wa MIICO, Catherine Mulaga alisema katika utatuzi wa migogoro ya wafugaji na wakulima wamefanikiwa kusaidia kupunguza migogoro iliyokuwepo katika kata za Mbalatse na Mfumbi kwa kiasi kikubwa, lakini changamoto kubwa waliyoibaini ipo kwa upande wa wanawake kumiliki ardhi.
"Tulifanya utafiti nakuona kwamba, kulikuwa na changamoto nyingi kwenye masuala ya ardhi ambayo yana athiri, ustawi wa maisha ya mkulima wilaya ya Makete, tulikuta kuna suala la uelewa mdogo wa sheria zinazoongoza masuala ya ardhi," alisema Grace.
"Changamoto nyingine ilikuwa ni kwa upande wa umiliki wa ardhi kwa mwanamke, suala la jinsia limekuwa likijitokeza ambapo wakinamama wengi wamekuwa wakiathiriwa kwenye upatikanaji wa ardhi," alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni