Jumanne, 28 Machi 2017

TAIFA STARS YAITANDIKA BURUNDI BAO 2-1 TAIFA LEO

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

Timu ya Taifa ya Tanzania "Taifa Stars' imefanikiwa kutoka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya timu ya Taifa ya Burundi kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika leo Jijini Dar es salaam.

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye dimba la Uwanja wa Taifa, timu ya Taifa Stars ndiyo ilikuwa ya Kwanza kuanza kufunga baada ya winga Simon Msuva kuipatia timu yake goli la kwanza katika dakika ya 20 akimaliza pasi safi ya Mohamed Hussein 'Tshabalala'.

Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza Taifa Stars walienda mapumziko wakiwa mbele kwa goli 1 - 0 dhidi ya Burundi.

Kipindi cha Pili kilianza kwa kila timu kulisakama lango la mwenzake na katika dakika ya 54, mshambuliaji wa Burundi Laudit Mavugo alitumia makosa ya beki kati Abdi Banda aliyepoteza mpira na kuifungia timu yake goli la kusawazisha.

Kocha Salum Mayanga anaamua kufanya mabadiliko mbalimbali kwa ikiwemo kumtoa Farid Musa na kuingia Mbaraka Yusuph ambaye aliweza kubadili matokeo na katika dakika ya 76 aliifungia Taifa Stars goli pili na la ushindi.

Mpaka dakika 90 zinamalizika Taifa Stars wanatoka kifua mbele kw goli 2-1 dhidi ya Burundi na inakuwa ni mchezo wa pili mfululizo kwa Taifa Stars kushinda baada ya mwishoni mwa wiki hii kuifunga Botswana kwa goli 2-0.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni