Jumanne, 28 Machi 2017

MAAFISA MAENDELEO YA JAMII WA MIKOA WAJENGEWA WELEDI KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO NCHINI

Na erasto ching’oro- Msemaji: Wizara ya Afya, 
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo imefungua kikao cha siku mbili cha Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa kwa ajili ya kuwajengea uwezo kuhusu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kuzuia na Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017-2022).

Akifungua kikao hicho, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Bw. Julius Mbilinyi ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia aliwashukuru Washirika wa Maendeleo katika kuhakikisha kuwa tatizo la ukatili dhidi ya wanawake na watoto linatokomezwa hapa nchini. Aliyataja mashirika haya kuwa ni pamoja na UN-WOMEN, Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Haki na Ustawi wa Watoto (UNICEF).

Mgeni Rasimi Kaimu Mkurugenzi wa Jinsia, aliwapongeza Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa shughuli mbalimbali ambazo wamekuwa wakizitekeleza katika maeneo yao ya kazi, juhudi ambazo zimekuwa na mchango katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini. Alifafanua kwamba, baada ya mafunzo haya, maafisa hao wataendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kupunguza ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021/20122.

Wanawake na watoto wamekuwa wakifanyiwa ukatili kwa kisingizio cha mila na desturi. Aidha, mfumo dume umesababisha wanawake kutoshiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu maendeleo yao, katika ngazi ya kitaifa, katika ngazi ya jamii na hata katika familia zao. Mara nyingi tumesikia wanawake na watoto wakipigwa, kubakwa na wakati mwingine kuuwawa na watu wa karibu. Vitendo hivi ni ukatili wa hali ya juu na vinaleta simanzi na madhara makubwa katika jamii yetu.

Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Julius Mbilinyi akifungua Kikao Kazi cha Maafisa wa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa (hawapo pichani) katika cha siku mbili kinachoanza leo katika Hotel ya Edema Mkoani Morogoro.
Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Julius Mbilinyi akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa wanaohudhuria kikao kazi kuhusu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto katika mkutano unaofanyika Hotel ya Edema Mkoani Morogoro.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha Maafisa Maendelo ya Jamaii wa Mikoa wakifuatilia maelezo ya wawezeshaji kuhusu utekelezaji wa Mpango Kazi wa taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto katika Hotel ya Edema, mkoani Morogoro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni