Jumanne, 28 Machi 2017

NEEMA WAMBURA AMSHUKURU RAIS MAGUFULI, AWAPONGEZA MADAKTARI NA WAUGUZI

Na John Stephen, MNH
Mgonjwa Neema Wambura ambaye alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) amemshukuru Rais John Pombe Magufuli baada ya afya yake kuimarika na kuruhusiwa leo kurejea nyumbani.
Neema amemshukuru rais kwa kumwezesha kupata matibabu tangu alipofikishwa katika hospitali hiyo Februari 23, mwaka huu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu amuepushe Rais Magufuli na mambo mabaya yote. Sasa nipata nguvu, nina furaha na naoga mwenyewe tofauti na awali,” amesema Neema.
Pia, Neema amewashukuru madaktari na wauguzi wa Muhimbili kwa kumpatia huduma bora na kumwezesha kupona majeraha ya moto.
Neema ambaye ni Mkazi wa Mkoa wa Mara alimwagiwa maji ya moto na mumewe wakati alipokuwa akichemsha maji kwa ajili ya kupika ugali na kuungua sehemu ya kifuani, shingo na mkono.
Mkuu wa Idara ya Upasuaji na Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dk Ibrahim Mkoma  amesema afya ya Neema inaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji sehemu ya shingoni ili kutenganisha shingo na sehemu ya kifua na kuziba majera ya moto.
“Neema anaendelea vizuri sasa anaweza kunyanyua shingo vizuri kabla ya hapo alikuwa hawezi kuinyanyua wala kuizungusha,” amesema.
Daktari bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dkt. Ibrahim Mkoma akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari kuhusu kuruhusiwa kwa mgonjwa aliyekuwa anapatiwa matibabu kutokana na majeraha ya kuunguzwa na maji ya moto kifuani, shingoni na mkononi, Bibi. Neema Mwita maarufu kama mgonjwa wa Magufuli. Neema alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali hiyo kufuatia msaada wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli baada ya kuguswa na taarifa za mgonjwa huyo mapema mwezi wa pili mwaka huu hali iliyompelekea kuchukua jukumu la kumsaidia.Mkuu wa Jengo la Sewahaji Bibi. Salome Mayenga (kushoto) na Mkuu wa Wodi namba 24 Sewahaji, Muhimbili Bibi. Georgina Kabaitileki.
 Dkt. Mkoma akionyesha  baadhi ya sehemu ambazo Neema amefanyiwa upasuaji  baada ya kupata majeraha makubwa baada ya kumwagiwa maji ya moto na mume wake huko mkoani Mara.
Neema Mwita akimshukuru Rais Dkt.  John Magufuli pamoja na wa watoa huduma wa  Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya afya yake kuimarika na leo ameruhusiwa kurudi nyumbani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni