Lowassa Ataja Vipaumbe vyake
13 Ndani ya Siku 100.
Mpekuzi blog
Mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa ametaja mambo 13 atakayoyafanya ndani ya siku 100 iwapo atachaguliwa kuwa Rais, huku akisema “atawakata kilimilimi” wanaombeza kuwa hawezi kuondoa umaskini wa wananchi.
Lowassa
alikuwa akihitimisha mikutano minne aliyofanya kwenye wilaya tatu za
Jiji la Dar es Salaam jana kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe.
Wakati
Lowassa akieleza hayo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
alitangaza azimio la Kawe lililobeba ajenda kuu tatu, ikiwamo ya kumtaka
Rais Jakaya Kikwete kutoa mwongozo wa jinsi Serikali yake
itakavyokabidhi madaraka kwa Ukawa kutokana na suala hilo kutokuwapo
kikatiba, huku mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitangaza mkesha
kwa wananchi siku ya kuamkia tarehe ya kupigakura na kutaka wanaume
wabakie kulinda kura zisiibiwe.
Akizungumza
kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya watu na viongozi wakuu wa
Ukawa, Lowassa alisema mambo hayo atayatekeleza kwa kasi ya kilometa
120 kwa saa.
Lowassa aliyataja mambo hayo kuwa ni;
- Uhakika wa dawa na vifaa vya uzazi wa akinamama.
- Umeme wa uhakika nchi nzima.
- Kupunguza foleni jijini Dar es Salaam.
- Kuondoa kero kwa wafanyabiashara wadogowadogo na waendesha bodaboda.
- Kumaliza tatizo la maji nchi nzima.
- Mfumo bora na rafiki wa wafanyabishara wakubwa na wadogo.
- Kufuta ada na michango kwa wanafunzi.
- Kupunguza kodi ya mshahara kwa wafanyakazi.
- Kufuta kodi zote za mazao ya wakulima.
- Mkakati wa kukuza michezo na sanaa.
- Kuunda tume ya kutatua migogoro ya wafugaji na wakulima.
- Kuanzisha kituo kila wilaya kwa ajili ya kutoa huduma za serikal.
- Kuboresha maslahi ya polisi, wanajeshi na walimu.
Mbali
na mambo hayo 13, aliahidi kumaliza kilio cha wananchi cha kupata
Katiba mpya inayotokana na maoni yao, akisema ni suala linalohitaji
kutuliza kichwa kulipatia ufumbuzi.
“Umaskini si mpango wa Mungu,” alisema Lowassa ambaye alikuwa akishangiliwa kwa nguvu. “Nina hasira ya kupambana nao na kuwaondoa Watanzania katika umaskini.”
Waziri
Mkuu huyo wa zamani aliyeihama CCM mwishoni mwa mwezi Julai, aligoma
kushuka jukwaani akitaka awekewe muziki acheze na maelfu ya wananchi
waliokuwa wakimsikiliza na kumkumbatia mkewe, Regina ambaye alifika
uwanjani hapo wakati mkutano huo ukikaribia kumalizika, kisha akambusu.
Awali, Lowassa alisema idadi ya kura anazohitaji ili ashinde urais ni milioni 14.
Akiwa
Mafinga mkoani Iringa, Lowassa aliomba wananchi wampigie kura milioni
10 ili awe Rais lakini jana alisema kuna haja ya kupata kura nyingi
iwezekanavyo ili ushindi wake usiathiriwe.
“Kilichonileta
hapa ni kuomba kura,” alisema Lowassa. “Naomba mnipigie kura milioni 14
na ushee ili ziweze kutosha kuwa Rais. Baada ya kupiga kura, wananchi
mnatakiwa kuzilinda ili zisiibwe.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni