Magufuli: Nitashusha bei ya saruji, mabati
Mpekuzi blog
Mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amesema endapo atachaguliwa, atashusha bei ya vifaa vya ujenzi vikiwamo saruji na mabati kuanzia mwakani akisema tayari kuna viwanda vikubwa ambavyo vimeshaanza kujengwa nchini.
Akiwahutubia wananchi wa Namtumbo, Ruvuma jana, Dk Magufuli alisema kuongezeka kwa viwanda hivyo akitolea mfano wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote ambacho kitakuwa kikubwa zaidi Afrika Mashariki na kuimarika kwa Barabara ya Songea – Masasi ambayo makandarasi wapo kazini, kutasaidia kuvutia wawekezaji na kusisimua biashara katika mikoa ya Kusini.
Akiwa Tunduru, Dk Magufuli aliahidi kuendeleza uchimbaji wa madini ya urani ili yaweze kuchochea maendeleo nchini.
Akiwahutubia wakazi wa Namtumbo wilayani Tunduru, Dk Magufuli alisema anafahamu bayana kuwa eneo hilo lina madini hayo hivyo akiingia madarakani, Serikali yake itaendeleza urani ili kuwasaidia kukuza uchumi wa wananchi hao.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa CCM mjini hapa, mgombea huyo alisema iwapo atapatiwa ridhaa hiyo Oktoba 25, ataimarisha uhusiano mzuri na nchi zote jirani na wafadhili wa maendeleo.
“Tutaendelea kuuenzi uhusiano mzuri na majirani zetu wanaotuzunguka wa Kenya, Malawi, Zambia, Msumbiji, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hadi Sudan Kusini. Pia, kuimarisha uhusiano na nchi nyingine za Afrika na mabara mengine na wafadhili wetu ambao wanatuamini sana na kutusaidia,” alisema Dk Magufuli.
Alisema wafadhili wengi wanachangia katika miradi ya maendeleo ya barabara kwa sababu wanaiamini Serikali na kuwa fedha hazitaliwa na mafisadi.
Alitokea mifano ya Barabara za Namtumbo – Tunduru-Mtambaswala zinazojengwa kwa ushirika na Shirika la Maendeleo la Japan (Jica) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kuwa ni matokeo ya uaminifu katika matumizi ya fedha za miradi.
“Wafadhili wanamwamini Magufuli kwa kuwa fedha zikitolewa hazichukuliwi. Hivyo msilete mtu ambaye haaminiki hata kwa wafadhili, akipatiwa fedha anakula, halafu akachukiwa na wafadhili baadaye wakasusia kutoa fedha za kumalizia miradi ya barabara tuliyoianza,”alisema.
Msafara wasimamishwa
Msafara wa mgombea huyo ulilazimika kusimamia mara nyingi baada ya wananchi kukaa barabarani kumtaka ajibu kero zinazowakabili, nyingi zikiwa ni za maji, barabara, umeme na afya.
Tangu alipoanza safari Songea Mjini, Dk Magufuli alisimama kwenye maeneo yasiyopungua 12, safari hii akitumia dakika chache tofauti na alivyofanya katika safari ya Vwawa-Tunduma mkoani Mbeya.
Dk Magufuli alivuta hisia za wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi wa Barabara ya Matemanga-Liuli aliposimama katika Kijiji cha Huria wilayani Tunduru kusikiliza kero zao zikiwamo za mishahara na kumuomba aendeshe mtambo wa kusawazisha udongo barabarani.
Baada ya kuujaribu mtambo huo kwa takriban dakika tano, aliwahakikishia kuwa mkandarasi SRBG atawalipa malipo yao yote kwa kuwa Serikali imeshamlipa fedha zote za mradi.
Akiwa Matemanga, aliwaahidi wananchi kujenga kiwanda cha kuongeza thamani za korosho kwa kuwa utawala wake utakuwa ni wa viwanda.
Huku akitumia historia ya utendaji wake katika Wizara ya Ujenzi, Dk Magufuli aliahidi kuwa Barabara ya Namtumbo-Masasi itakamilika mwakani na kuwa kuna makandarasi wanane wanaoendelea na kazi za ujenzi.
Katika mkutano wake Mjini Tunduru, Dk Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti mtarajiwa wa CCM, aliwapokea makada wapya 16 waliodai kuitosa Chadema.
Kutokana na kusimama mara kwa mara njiani kuzungumza na wananchi, Dk Magufuli alilazimika kufanya mikutano mifupi zaidi mjini Masasi huku akiwaomba radhi wakazi wa mji huo kwa kuchelewa.
“Ninafahamu wananchi wa Masasi mna masikitiko makubwa ya mazao, korosho, stakabadhi ghalani, ninataka niwaahidi hili nitalighulikia,”aliuambia umati mkubwa wa wananchi katika Uwanja wa Boma na kuongeza:
“Waziri wangu nitakayemteua wa kilimo hili lazima alifanyie kazi.”
Aliwaahidi wakazi wa mji huo kuwa atajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Masasi hadi Mtwara kupitia Newala yenye urefu wa kilomita 200.
Alisema tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara hiyo vimeshafanyika na kilichobaki ni kuanza tu kujengwa kwa kuwa tenda ilishatangazwa.
Alisema kujengwa kwa barabara hiyo na nyinginezo kuiwezesha Tanzania kuwa ya kisasa.
Aliendelea kutoa ahadi ikiwamo ya mikopo ya Sh50 milioni kwa vikundi vya vijana na wanawake katika kila kijiji, kujenga reli ya kisasa ya Mtwara-Mbamba Bay na kuwasomesha bure, watoto kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
Kutokana na ufupi wa muda, Dk Magufuli aliahidi kurejea Masasi endapo atachaguliwa ili kufanyia kazi masuala mbalimbali yakiwamo ya maji na mengineyo.
“Ni bahati mbaya ndugu zangu nimefika jioni nisameheni sana nitakuja tena na Mungu awabariki sana,” alimaliza kwa salamu ya Masasi “hoyee”, “Masasi kucheleeee.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni