TENDO LA HISANI LA WAPENDELEVU’89 KWA OCEAN ROAD CANCER INSTITUTE
Wapendelevu’89 ( WaP89) ni kikundi cha Wanawake waliomaliza Kidato cha sita Mwaka 1989 katika Shule ya Wasichana Weruweru. Kikundi hiki kinaundwa na wanachama 44 ambao wanajishughulisha na ujenzi wa Taifa katika Nyanja mbalimbali wakiwamo madaktari, wahasibu, wahadhiri, wachumi, walimu/wahadhiri na wafamasia.
Kutokana na kuwa kwao sehemu ya Jamii , na kuona ombwe lililopo katika sehemu mbalimbali na hasa katika huduma za jamii na pia kuthamini uwajibikaji wa pamoja, kikundi kiliona ni vema katika mipango yake (Work Plan) ya mwaka 2015 kifanye tendo la Hisani kwa jamii -hitaji. Ndipo wazo la kusaidia eneo la ORCI, (Taasisi ya Saratani ya Ocean Road) lilipozaliwa na ukamilifu wake ukawa hapo tarehe 23 Mei 2015.
Katika tukio hili Kikundi kilikabidhi msaada wenye thamani ya takribani TShs. Milioni 12 uliotokana na michango binafsi ya kikundi pamoja na kuungwa mkono na wadau wengine wenye mapenzi mema.
Tukio hili lilijumuisha utoaji wa vitu kwa wagonjwa wenyewe hapo hospitalini ambapo wanakikundi walikabidhi kwa mgonjwa mmoja mmoja vifaa vya matumizi binafsi, ambapo jumla ya wagonjwa waliokabidhiwa walikuwa 231 ( 68 akinababa na 163 kinamama). Lakini vile vile WaP’89 walikabidhi vifaa mbalimbali kwa wizara kupitia mwakilishi wake Dk. Shadrack Busweru
WaP89 wakiwa na Mh. Alshaymaar Kwegyir, Mbunge wa Viti maalum ( Walemavu) wakiwa katika Taasisi yay a Saratani Ocean Road wakipanga vitu tayari kwa ugawaji katika wodi ya Wanaume.
Msaada huu umeainishwa kama ifuatavyo :
ü Mashuka 500 ya kutumiwa na wagonjwa
ü Mito ( pillows) ya wagonjwa
ü Dawa za kupunguza maumivu kwa wagonjwa wanaopokea tiba hapo ORCI
ü Nauli kwa wagonjwa walioruhusiwa lakini wanashindwa kwenda nyumbani ( mikoani)
ü Sabuni, nguo na vifaa vya kuhifadhia chakula.
Awamu ya pili ya ugawaji wa nguo kwa wagonjwa katika Wodi ya Wanawake. Mh. Al Shaymaar Kwegyir akisubiri mzigo wake wa kugawa huku akipata maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa WaP89 Stella ¬Emma Katende ( katikati)
Mgeni rasmi ambaye alijumuika na WaP’89 katika zoezi zima alikuwa Mbunge wa Viti Maalum (Walemavu) Mh. Al Shaymaar Kwegyir ambaye aliwapongeza sana Wapendelevu’ 89 kwa moyo wao wa kuijali jamii na hasa ukizingatia kuwa wamama hawa ni watu wenye shughuli zao nyingi na hivyo kutoa muda na raslimali ni jambo la kutia moyo sana.
Vile vile Mh. Kwegyir alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watu wengine kusaidia jamii na hasa wagonjwa hawa ambao wanakuwa na tiba za muda mrefu. Vile vile katika nafasi yake ya Mbunge anayewakilisha Jamii ya watu wenye ulemavu, kutilia mkazo umuhimu wa watu wenye ulemavu wa ngozi ambao nao huathiriwa sana na Saratani ya ngozi kutokana na athari za jua katika nchi yetu ambayo iko karibu na Ikweta, kuwahi tiba hospitali mara waonapo dalili za awali kama vipele katika ngozi zao ili kuepuka madhara makubwa kwenye ngozi na afya zao mara vipele hivi vigekapo saratani.
Akina mama wanachama wa WaP89 wakiwa na mgeni rasmi Mbunge wa Viti maalum Mh. Alshaymaar Kwegyir ( mwenye miwani) na Mwakilishi wa Wizara ya Afya ( Idara ya Magonjwa Yasiyoambukiza), Dr Shadrack Busweru ( mwenye shati Jeupe) wakati wa makabidhiano ya vifaa mbalimbali vilivyotolewa na Kikundi cha WaP89 kwa hospitali ya Ocean Road, Dar Es Salaam hivi karibuni.
WaP89 na mgeni rasmi Mh. Alshaymaar Kwegyir wakiwa katika picha ya pamoja katika hospital ya Ocean Road mara baada ya kukamilisha zoezi la ugawaji wa vifaa kwa wagonjwa
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni