KAULI YA RC KANDORO JUU YA MJAMZITO ALIYENYANYASWA HOSPITALI YA META JIJINI MBEYA
SAKATA la unyanyasaji aliofanyiwa mwanamke mjamzito Judith Komba siku ya kujifungua katika hospitali ya Rufaa kitengo cha wazazi cha Meta limechukua sura mpya baada ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro kuagiza wauguzi waliokuwa zamu siku ya tukio wachukuliwe hatua stahiki.
Mnamo usiku wa Mei 13 mwaka huu mwanamke Judith Komba mkazi wa Iwambi jijini Mbeya alijikuta analazimika kujifungulia katika kitanda cha kubebea wagonjwa ndani ya hospitali ya Meta pasipo usaidizi wa mtu yeyote na mtoto kunusurika kifo kutokana na mazingira hatari yaliyoukabili uzazi wake.
Hivi karibuni Judith alikaririwa na vyombo vya habari akibainisha kuwa alilazimika kujifungulia kwenye mazingira hayo baada ya kuwafuata mara kadhaa wauguzi waliokuwa akiwaomba wamsaidie lakini walimpuuza na wakaendelea kulala kwenye chumba chao.
Mwanamke baada ya kuzidiwa na kujikuta hawezi kurejea wodini alikokuwa amelazwa alijikuta analazimika kulala kwenye kitanda cha kubebea wagonjwa akiwa amezidiwa na uchungu na akajifungulia hapo.
Hatua hiyo imeonesha kusononesha wadau wengi akiwemo mkuu wa mkoa wa Mbeya ambaye amemuagiza katibu tawal mkoa kufuatilia suala hilo na kuwachukulia hatua stahili wauguzi waliokuwa zamu.
Kandoro alitoa agizo hilo kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa mpango wa miaka minne wa Kusaidia maisha ya Akina mama wajawazito na Watoto kwa halmashauri 10 za mkoani Mbeya unaofadhiliwa na shirika la Korea International Cooperation Agency(KOICA) kupitia Unicef.
Kandoro alisema yapo majibu rahisirahisi yaliyotolewa na utawala wa hospitali hiyo lakini ukweli ni kuwa majibu hayo hayatoshelezi hata kidogo ikilinganishwa na uzembe uliotokea siku hiyo.
“Majibu yametolewa kirahisi rahisi.Mimi nasema siyakubali na naagiza katibu tawala uhakikishe unafuatilia jambo hilo na waliohusika wawajibishwe.Kwani hawafahamiki waliokuwa zamu siku hiyo?Kwa nini utawala utumie lugha rahisi rahisi”
“Hatuwezi kuruhusu mtu atoe matatizo yake nyumbani kwake ayalete kazini na kuwaumiza wasio husika na matatizo hayo.Tumeambiwa hapa moja ya vitu vinavyochangia vifo vya wajawazito na watoto wachanga ni uzembe wa watoa huduma.Hili lazima tulifanyie kazi haraka” alisema Kandoro.
Chanzo Lyamba Lya Mfipa |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni