Hotuba Ya Mh. Edward Lowassa Aliyoitoa LEO jijini Arusha Wakati Akitangaza Nia Ya Kuomba Kuteuliwa na CCM Kuwa Mgombea Urais Wa Tanzania
Mtangaza nia ya kuwania Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mh. Edward Lowassa akiwapungia mkono maelfu ya wananchi waliofurika kwa wingi kwenye Uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid,jijini Arusha jioni ya leo, wakati wa kutangaza nia yake hiyo ya kuwania Urais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mtangaza nia ya kuwania Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mh. Edward Lowassa akiwapungia mkono maelfu ya wananchi waliofurika kwa wingi kwenye Uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid,jijini Arusha jioni ya leo, wakati wa kutangaza nia yake hiyo ya kuwania Urais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Mh. Kangi Lugola akisalima umati wa watanzania uliofurika kwa wingi kwenye Uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid,jijini Arusha jioni ya leo, kumsikiliza Mtangaza nia ya kuwania Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mh. Edward Lowassa (kulia).
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Ndg. Onesmo Ole Nangole akizungumza machache kabla ya kumkaribisha Mtangaza nia ya kuwania Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mh. Edward Lowassa, kwenye Uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid,jijini Arusha jioni ya leo.
Mh. Lowassa akiwapungia wananchi.
Mtangaza nia ya kuwania Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mh. Edward Lowassa akihutubia katika mkutano wa hadhawa wa kutangaza nia yake hiyo, kwenye Uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid,jijini Arusha jioni ya leo.
Mh. Edward Lowassa akiteta jambo na Mkewe Mama Regina Lowassa wakati wa mkutano uliofanyika jioni ya leo kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Mh. Edward Lowassa akipongezwa na baadhi ya Wabunge waliohudhulia mkutano huo, baada hotuba yake.
PICHA ZOTE NA MICHUZI |
UTANGULIZI:
Ndugu
zangu wana-CCM na Watanzania wenzangu,
Hii ni
siku muhimu kwangu na kwa nchi yetu. Leo nimeamua kuwaita ili kuwatangazia
rasmi Watanzania wenzangu azma yangu ya kutaka kuomba ridhaa ya chama chetu,
Chama Cha Mapinduzi (CCM), niweze kuteuliwa kuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Nasema
hii ni siku muhimu kwangu kwa sababu naamini historia yangu itainakili kama ni
siku ambayo kwa mara ya pili katika maisha yangu nimejitokeza kuwania kuiongoza
nchi yetu kupitia chama chetu. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1995 wakati wa
uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi hapa nchini nilipojitokeza nikiwa pamoja na
Rais Jakaya Kikwete; wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Tulikwenda
pamoja kuchukua fomu ndani ya Chama na baadaye tukafanya mazungumzo ya pamoja
na waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo
halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati ya
wawili sisi basi mwenzake ambaye hatafanikiwa angemuunga mkono.
Ningeweza
kujitokeza tena mwaka 2005 lakini nikaamua kwa dhati kabisa kumuunga mkono moja
kwa moja Rais Jakaya Kikwete.
Nikiwa
Mwenyekiti wa Kampeni niliwaongoza wenzangu kufanikisha ushindi mkubwa wa
mgombea tuliyemuunga mkono na baadaye ushindi mkubwa wa asilimia 80 wa Chama
Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi mkuu wa 2005.
Nitaeleza
kwa nini nimeamua kujitokeza tena mwaka huu na kwa nini naamini mimi ndiye mtu
sahihi wa kuiongoza nchi yetu wakati huu. Mpaka hapa itoshe tu kuwaeleza ni kwa
kwa nini naamini leo ni siku muhimu kwangu.
Lakini
nasema ni siku muhimu kwa nchi yetu pia. Nasema hivyokwa sababu naamini inajibu
wito wa mahitaji ya sasa ya uongozi wa Taifa letu wa kumpata kiongozi imara
atakayewaongoza Watanzania kujenga taifa imara. Na hili pia nitalieleza kwa
kina.
Hali ya Nchi na Matarajio ya
Watu:
Miaka
48 iliyopita katika jiji hili la Arusha, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage alianzisha mchakato wa kujenga taifa huru kiuchumi na kupiga vita
maadui umaskini, ujinga na maradhi kwakutumia silaha ya kujitegemea.
Leo
hii, wakati taifa likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu ujao, hatuna budi kutafakari
tulikotoka, tulipo na tunapotaka kwenda ili tuweze kubuni upya mikakati ya
kuhitimisha azma aliyo kuwa nayo Mwalimu, ili tujenge taifa huru, lenye
utulivu, mshikamano, amani na maendeleo.
Nchi
yetu hivi sasa inapita katika kipindi kigumu cha mpito katika maeneo yote makuu
ya maisha yetu – katika siasa, katika uchumi na katika maisha ya kijamii.
Kisiasa,
tumeshuhudia kuongezeka kwa vuguvugu la mfumo wa vyama vingi ambapo ushindani
kati ya vyama vya siasa unazidi kuwa mkali na kwa bahati mbaya kufikia sura ya
kuonekana kama vile ni mapambano ya watu binafsi badala ya mapambano ya sera na
dira ya kuongoza nchi.
Tunashuhudia
kuongezeka uhasama binafsi kati ya wanasiasa ndani ya chama kimoja kimoja na
pia kati ya wanasiasa wa chama kimoja dhidi ya kingine. Kadiri siku
zinavyokwenda, hali inazidi kuzorota na ikiachiwa kuendelea nchi yetu inaweza
kujikuta mahali pabaya.
Kukua
kwa ushindani ni jambo jema linalokomaza na kurutubisha demokrasia yetu na
tukiwa na ushindani wenye afya unaweza kuwa chachu ya kuleta mabadiliko mema
kwa wananchi na kupelekea kuongezeka kwa kasi ya maendeleo ya kiuchumi na
kijamii katika nchi yetu.
Kinyume
chake ushindani unaochukua sura ya chuki binafsi au kukomoana na hata
kulipizana visasi si ushindani wenye tija na tunapaswa kuutafutia tiba.
Tunahitaji
uongozi imara kusimamia kipindi cha mpito kutoka siasa muflisi za aina hii na
kuelekea kwenye siasa mpya zinazoimarisha ushindani wenye tija unaojikita
katika kushindana katika kuwapatia huduma bora Watanzania.
Kiuchumi,
tumeshuhudia ukuaji mzuri na kuongezeka kwa mapato ya ndani ya Serikali na
uimarishaji wa mfumo wa uwajibikaji na ulipaji kodi.
Kwa
upande mwengine, Serikali ya Rais BenjaminiMkapa na Rais Jakaya Kikwete
imefanya kazi kubwa katika uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi asilia ambapo
kiwango kikubwa cha gesi asilia kimegunduliwa.
Tanzania
sasa imekuwa ni miongoni mwa nchi zinazovutia uwekezaji mkubwa katika sekta
hiyo ambayo inatajwa kwamba inaweza kuja kubadilisha kabisa maisha ya
Watanzania.
Hata
hivyo, kipindi hiki cha mpito kuelekea ujenzi wa uchumi wa kisasa kimeshuhudia
kuongezeka kwa hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi kwamba hawatonufaika
naukuaji huu wa uchumi na ugunduzi wa utajiri mkubwa wa gesi asilia.
Kwa
upande mwingine, vijana wanataka kuona ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa utajiri
huo unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira zenye maana ili waweze
kukabiliana na changamoto za maisha yao.
Niliwahi
kusema kwamba tatizo la ukosefu wa ajira likiachiwa bila ya kutafutiwa ufumbuzi
imara ni bomu linalosubiri kulipuka.
Vijana
wasio na ajira hupoteza matumaini na ni rahisi kughilibiwa kuingiza nchi katika
machafuko.Tunahitaji uongozi imara kuweza kuikabili hali hiyo na kuitafutia
suluhisho maridhawa.
Kijamii,
kipindi cha karibuni tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya tabia miongoni mwa raia
katika hali ambayo haijawahi kuwa sehemu ya utamaduni wa Watanzania.
Kumekuwa
na ongezeko la kutisha la matukio ya uhalifu linalokwenda sambamba na wananchi
kuonyesha wanapoteza imani na taasisi zinazosimamia sheria na usalama na kuamua
kujichukulia sheria mikononi mwao.
Kumeripotiwa
matukio mengi yakiwemo ya kuvamiwa vituo vya polisi, askari kupigwa na kuporwa
silaha, matumizi makubwa ya nguvu katika utatuzi wa migogoro mbalimbali hasa
ile ya kijamii, mathalani migogoro ya wakulima na wafugaji, mivutano ya kidini
na pia mivutano baina ya viongozi wa dini wenyewe kwa wenyewe na baina ya
viongozi wa dini na wale wa Serikali.
Matokeo
yakemshikamano wa taifa nao unaingia majaribuni. Mara nyingine wananchi
wanatuuliza viongozi iwapo hii ndiyo nchi tuliyoachiwa na waasisi wetu.
Tunahitaji uongozi imara wa kukabiliana na changamoto hizi na kurudisha
mshikamano wa taifa letu na watu wake.
Watanzania Wanataka Mabadiliko;
Ndugu
zangu, mnaweza kujiuliza kwa nini nimeyaeleza yote hayo na yana mahusiano gani
na dhamira yangu ya kutangaza nia ya kutaka kuiongoza nchi yetu kupitia CCM?
Nimeyaeleza
haya kwa sababu haya na matukio mengine yanayoendelea nchini yamepelekea
Watanzania kutaka mabadiliko.
Watanzania
wanataka mabadiliko yatakayowawezesha kuzishinda changamoto hizi na kuwaongoza
kujenga Taifa imara ambalo kila mwananchi wake anaishi akiwa na uhakika wa
mahitaji yake muhimu na papo hapo akijiridhisha kwamba leo yake ni bora kuliko
jana yake, na kesho yake itakuwa bora zaidi kuliko leo yake.
Kwa
maneno mengine, Watanzania wanahitaji mabadiliko yatakayowapa uongozi imara
unaoweza kuwaongoza kujenga taifaimara. Hii ndio Safari ya Matumaini.
Chama
chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), na watangulizi wake, TANU na ASP, kimepata
bahati ya kuungwa mkono na Watanzania tokea enzi za kupigania uhuru, wakati wa
Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar, na pia miaka yote tokea Uhuru,
Mapinduzi na hatimaye Muungano wetu. Watanzania hawajawahi kushuhudia chama
kingine kikiongoza Serikali zetu zaidi ya CCM. Wamekiamini na wanaendelea
kukiamini.
Hata
katika yale majimbo machache ya nchi yetu ambayo hatukufanya vizuri katika
uchaguzi, ukiangalia kwa undani utaona si kwamba watu wa maeneo hayo wana
matatizo na CCM kama Chama bali wana matatizo na baadhi ya viongozi ambao
walishindwa kukiwakilisha vyema Chama na kutambua matakwa ya wananchi hao.
Mimi
naamini kwamba hata katika kipindi hiki ambapo Watanzania wanaonekana kutaka
mabadiliko bado wanaendelea kuamini kwamba watayapata mabadiliko hayo ndani ya
CCM.
Lakini
kama alivyotupa wasia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1995 wakati
wa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi hapa nchini,
Watanzania wasipoyapata mabadiliko hayo ndani ya CCM watayatafuta nje ya
CCM.
Mimi
naamini kwamba CCM tunao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka.
Tuwape imani na imani hiyo iwe ni ya dhati na ya ukweli kwamba CCM inao uwezo
wa kuwapa uongozi imara wanaouhitaji kwa ajili ya kujenga taifa imara.
Vyama
vya siasa vinajumuisha watu na vinaongozwa na watu. Moja ya hulka ya binadamu
ni kubadilika kulingana na mahitaji ya mazingira anayoishi.
Kwa
maneno mengine, binadamu ni ‘dynamic’. Kwa sababu hiyo basi, hata vyama vya
siasa vinapaswa kuwa ‘dynamic’.
CCM
haijapata kuwa na upungufu wa sifa ya ‘dynamism’. Kwa zaidi ya miongo mitano
sasa, CCM (na kabla yake TANU na ASP) iliweza kubadili dira na mwelekeo wake
ili kwenda sambamba na mahitaji ya Watanzania ya wakati husika.
Ndiyo
maana tumepita katika vipindi tofauti vya mpito kwa mafanikio makubwa licha ya
changamoto nyingi zilizotukabili.
Tanzania
imeendelea kuwa nchi ya amani licha ya kubadili mfumo wetu wa siasa kutoka ule
wa chama kimoja kuja vyama vingi; licha ya kubadili mwelekeo wa uchumi wetu
kutoka ule wa dola kumiliki njia zote kuu za uchumi kuja katika uchumi wa soko
unaozingatia ushiriki mpana wa Watanzania wa matabaka yote; na hata karibuni
kabisa katika mchakato wa kuipatia nchi yetu Katiba mpya.
Tanzania
tumeweza kufanya mabadiliko ya uongozi mara nne katika hali ya amani na
maelewano, jambo ambalo nchi nyingi za Afrika zimeshindwa.
Ni
imani yangu kwamba tukijikubalisha tunaweza tena kuwapa Watanzania
wanachokitaka katika zama hizi za sasa.
Lakini
ni lazima tuoneshe dhamira hiyo kwa dhati ili, kama alivyotuasa Mwalimu
Nyerere, Watanzania wasiyatafute mabadiliko hayo nje ya CCM.
Nasisitiza
tena kwamba CCM inao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka, lakini
pia wananchi wana hiali kuchagua mabadiliko wanayoyataka.
Uongozi unaohitajika kuleta mabadiliko
yanayotakiwa:
Rais
Jakaya Kikwete amefanya kazi kubwa katika kipindi chake na kama ambavyo amekuwa
akisisitiza mara kwa mara katika hotuba zake za karibuni ni kwamba yeye ametekeleza
wajibu wake kwa kuweka misingi imara ya ujenzi wa Taifa la kisasa lenye uchumi
madhubuti na unaoweza kukua kwa kasi.
Amesema
anamwachia atakayemkabidhi uongozi wa nchi yetu baada ya yeye kumaliza muda
wake kuendeleza pale atakapoachia.
Kwa maoni
yangu ili kuifanya kazi hiyo na kuzikabili changamoto nilizozieleza, nchi yetu
inahitaji uongozi wenye sifa zifuatazo:
-
Uongozi wenye uthubutu, usioogopa kufanya kufanya maamuzi magumu;
-
Uongozi thabiti na usioyumba;
-
Uongozi makini na mahiri;
-
Uongozi wenye ubunifu na wenye upeo mkubwa;
-
Uongozi utakaozikabili changamoto kifua mbele na siyo kuzikimbia;
-
Uongozi unaoamini katika mfumo shirikishi katika ujenzi wa Taifa;
-
Uongozi unaozingatia muda katika kutekeleza majukumu yake.
Naamini
pia kwamba wananchi wanataka Rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe
na sifa kuu zifuatazo:
-
Aweze kuwaunganisha Watanzania (kukabiliana na viashiria vya migawanyiko ya
aina mbali mbali inayoinyemelea Tanzania);
-
Aweze kuja na sera na mikakati ya kuinua uchumi wa Tanzania na kukuza pato la
Mtanzania;ikiwemo kupunguza tofauti ya kipato kati ya aliyekuwanacho na
wasiokuwanacho;
-
Aweze kuja na sera na mikakati ya kuzalisha ajira kwa vijana wetu;
-
Aweze kutokomeza mianya ya rushwa kwa vitendo;
-
Aweze kuwa mfano wa kuchapa kazi na kuwajibika;
-
Asimamie nidhamu ya matumizi ndani ya Serikali;
-
Aweze kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali;
-
Aweze kutumia fursa yetu ya kijiografia kibiashara
Uongozi Imara,Taifa Imara
Naamini
kwamba uongozi wa juu wa nchi katika nafasi ya Urais si kazi ya lelemama na
unahitaji utashi. Kabla hata ya kutakiwa na wenzako ni lazima kwanza wewe
mwenyewe uamini na uwaaminishe wenzio kwamba unao uwezo wa kuwaongoza wananchi
wenzako. Na katika hilo, rekodi yako ni lazima izungumze na kulithibitisha
hilo.
Binafsi
nina hazina ya uzoefu na rekodi njema ya matokeo ya kazi nilizozifanya katika
uongozi na utumishi wa umma ndani ya CCM na ndani ya Serikali. Nilianza kazi
nikiwa Katibu Msaidizi wa CCM katika mikoa ya Shinyanga, Arusha na Moshi.
Nimekuwa
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu ya CCM. Niliingia Bungeni
mwaka 1985 na baadae mzee wangu, Rais Ali Hassan Mwinyi, akaniamini kwa
kuniteua kuwa Waziri.
Nimekuwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Ardhi, Makaazi na Maendeleo ya
Miji, Waziri wa Mazingira, Waziri wa Maji na hatimaye Waziri Mkuu.
Miongoni mwa mafanikio ninayojivunia katika uongozi na utumishi
wangu, na
ambayo Watanzania wanayatambua na naamini wanayathamini, ni pamoja na:
-
Nikiwa Waziri wa Maji chini ya uongozi mahiri wa Rais Mkapa,tulithubutu
kushawishi na kuongoza hatua za kukataa kufungika na makubaliano yaliyowekwa na
wakoloni ambayo yalikuwa yanazizuia nchi zilizopakana na Ziwa Victoria zisiweze
kufaidika ipasavyo na maji ya Ziwa hilo. Leo hii ndugu zangu wa Kanda ya Ziwa
wanafaidika na ujasiri wetu katika kukabiliana na suala hilo zito.
-
Nikiwa Waziri wa Mazingira, tulipanda miti mingi zaidi kuliko wakati mwingine
wowote tokea Uhuru na pia kuwakabili kikamilifu na kuwachukulia hatua
waliochafua na kuharibu mazingira.
-
Nikiwa Waziri Mkuu, tulisimamia agizo la Rais Kikwete na kufanikisha
utekelezaji wake ndani ya miaka miwili kwa kujenga shule nyingi za sekondari
kuliko wakati mwingine wowote tokea Uhuru.
-
Kipindi hicho hicho, tulisimamia agizo la Rais Kikwete la kuanzisha Chuo Kikuu
cha Dodoma na kuhakikisha kinakamilishwa kwa wakati. Leo hii Chuo Kikuu hicho
ni fahari ya Tanzania.
Tunapomtafuta
Rais wa Jamhuri ya Muungano ni lazima tukumbuke kwamba tunamtafuta mtu ambaye
atakuwa pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika nchi
yetu. Na kwa Chama Cha Mapinduzi tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia Mwenyekiti
wa Chama chetu.
Naamini
kwa vigezo vyote, nina kila sifa ya kubeba dhamana hizo nzito. Katika mambo
ambayo najivunia na sitoyasahau katika historia yangu ni kushiriki kwangu
kuilinda nchi yangu pale ilipohitajika.
Nilishiriki
kikamilifu katika Vita vya Kagera nikiwa miongoni askari wa mstari wa mbele wa
mapambano. Nikiwa Mbunge nilipata heshima ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama. Naamini Watanzania hawatakuwa na wasiwasi wa usalama wao
nikiwa Amiri Jeshi Mkuu.
Nimeeleza
uzoefu wangu kwenye Chama na huo hauhitaji maelezo zaidi. Ninakijua vyema Chama
Cha Mapinduzi kiasi cha kutosha kabisa kukiongoza kama Mwenyekiti wake pale
wakati utakapofika.
Wana-CCM
wanajua nikikabidhiwa uongozi, Chama chetu kitakuwa chini ya nahodha madhubuti,
mzoefu na asiyeyumba.
Kutokana
na rekodi yangu hii, naamini ninazo sifa za kuwaongoza Watanzania wenzangu
katika zama mpya za ujenzi wa Taifa la kisasa lenye watu wazalendo
walioshikamana na lenye uchumi imara unaomnufaisha kila Mtanzania. Naamini
ninao uwezo wa kuwapa Watanzania Uongozi imara kwa ajili ya ujenzi wa Taifa
Imara.
Dira yangu na Matarajio ya
Watanzania
Mfumo
tuliojiwekea hapa nchini unaelekeza kila chama cha siasa kinachosimamisha
mgombea Urais na kinachowania kuongoza nchi yetu kuja na Ilani ya Uchaguzi
ambayo ndiyo inayoweka misingi ya sera zitakazofuatwa na Serikali
itakayoongozwa na chama hicho pale kinapopewa ridhaa ya kuongoza nchi.
Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa ni cha kupigiwa mfano katika kutayarisha Ilani
bora na ndiyo maana mara zote kimepewa ridhaa ya kuongoza nchi yetu. Tumefanya
hivyo tokea enzi za mfumo wa chama kimoja na tumeendelea kufanya vizuri katika
mfumo wa kushindanisha sera kupitia vyama vingi.
Najua
kwamba Ilani ya CCM ya mwaka 2015 imo katika hatua za mwisho za kukamilishwa na
itakapopata baraka za vikao vya Chama itakuwa ndiyo msingi wa utendaji wa
Serikali ya Awamu ya Tano itakayochaguliwa Oktoba mwaka huu.
Hata
hivyo, naamini pia kwamba mgombea mwenyewe anayetaka ridhaa ya Chama na ya
Watanzania kuongoza nchi naye anapaswa kueleza dira yake.
Mimi,
baada ya kutafakari kwa kina changamoto tulizo nazo na matarajio na matumaini
waliyo nayo Watanzania, naamini kwambaUongozi imara unaolenga kujenga Taifa imara
unapaswa kuwa na dira yenye malengo yafuatayo:
-
Kuimarisha Muungano wetu kwa kuyashughulikia yanayotutenganisha na kuyafanyia
kazi ili yasivuruge yale yanayotuunganisha ambayo ni mengi zaidi na makubwa
zaidi.
-
Kushughulikia matumizi mabaya ya siasa za udini na ukabila kwa kuimarisha siasa
zilizoshiba uzalendo na zenye kutuelekeza kwenye Utanzania wetu.
-
Kujenga uchumi imara na wa kisasa, na ambao ni shirikishi unaomnufaisha kila
Mtanzania aliyeko mjini au kijijini. Tunapaswa kubadili hali tuliyo nayo sasa
ambapo Kilimo kinaonekana kama kimesahauliwa na wakulima wetu wanaonekana
wanakata tamaa.
Wafugaji
na wavuvi nao wanahisi sekta zao hazijapewa umuhimu unaostahiki. Tunahitaji
kuondokana na hali iliyopo sasa ya kuwa Taifa linalouza malighafi na badala
yake kuwa Taifa linalosindika na kusarifu mazao na kutengeneza wenyewe bidhaa
zitokanazo na malighafi yake.
Ndani
ya miaka mitano ijayo tutahakikishatunaiondolea Tanzania sifa ya kusafirisha
malighafi na badala yake kusindika mazao yanayozalishwa hapa nchini kama pamba,
kahawa, chai na korosho na kuyaongezea thamani (value addition).Mkakati huu utazalisha
ajira nyingi na kuongeza mapato ya fedha za kigeni nchini.
Tunahitaji
kujielekeza kwenye kujenga viwanda na kuleta ajira. Tuna vivutio vingi sana vya
utalii lakini bado Tanzania inapitwa na nchi kama Afrika Kusini katika kuingiza
idadi kubwa ya watalii.
Kwa
nini nchi kama Dubai iweze kuvutia watalii kwa mamilioni na Tanzania tushindwe?
Tunapaswa kukabiliana kikamilifu na hisia zilizopo miongoni mwa wananchi kwamba
Tanzania hainufaiki ipasavyo na utajiri wa rasilimali zake nyingi ilizo
nazo.
Tutajipanga
zaidi kuhakikisha tunanufaika kama nchi na rasilimali zetu kama madini na gesi
asilia. Hii ndio Safari ya Matumaini
-
Kukuza kipato cha wananchi na kunyanyua hali za maisha ya watu wetu. Tunapaswa
kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi tunaouzungumzia unamnufaisha Mtanzania
aliyeko mjini au kijijini na kwamba hali za Watanzania wa matabaka yote
zinanyanyuka na kwamba wanaridhika na kuuona uhalisi wa ukuaji wa maendeleo
tunayoyazungumzia.
-
Kuondokana na sifa mbaya ya kuwa Taifa ombaomba. Kwa wingi wa rasilimali tulizo
nazo na neema ya ardhi, maziwa, mito na bahari Tanzania tuna kila sababu ya
kuacha kuwa ‘bakuli la ombaomba’ na badala yake kuwa ‘mkoba wa neema’ katika
Afrika.We can transform our nation from being the begging bowl to become the
bread basket of Africa.
-
Kujenga mfumo mpya wa elimu unaojielekeza kuwatayarisha vijana wetu waweze
kuajirika, kujiajiri na kushindana katika soko la ajira.
Tumepiga
hatua kadhaa katika elimu lakini kiwango cha elimu bado ni hafifu. Pamoja na kuwa
na shahada (degrees), bado wahitimu wetu hawawezi kushindana kwenye soko la
ajira.
Wakati
tunazungumzia kuunganisha soko la ajira katika Afrika Mashariki,hatuna budi
kujikita kubadili mfumo wetu wa elimu na kuuelekeza kwenye mafunzo ya ufundi na
stadi yanayowajenga wahitimu wetu kuwa wabunifu na wenye kujiamini katika
kukabiliana na changamoto za maendeleo duniani.
-
Kuhakikisha tunakabiliana ipasavyo na kulipunguza kwa kiasi kikubwa kama si
kulimaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama. Ni jambo la
kusikitisha kwamba tumezungukwa na mito na maziwa lakini bado watu wetu hawana
maji ya kunywa hata ndani ya Dar es Salaam.
-
Kujenga na kusimamia mfumo imara wa kutekeleza sera na sheria tunazozitunga na
kuzipitisha kwa lengo la kumtumikia Mtanzania na kumjengea uwezo wa kubadili
maisha yake ili tuweze kwenda sambamba na viwango vya kimataifa. Tanzania
imepata sera na sheria nzuri sana lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu.
Tumekuwa
wepesi wa kutunga sera na sheria lakini wazito mno wa kuzitekeleza na
kuzisimamia. Uongozi imara wenye kulenga ujenzi wa Taifa imara utahakikisha
tunakuwa mfano wa utekelezaji wa sera na sheria tulizo nazo na mpya
zitakazotungwa kukabiliana na malengo tuliyojiwekea.
Mambo
haya niliyoyaeleza hapa ndiyo yatakayokuwa msingi mkuu wa utendaji wa Serikali
nitakayoiongoza pale nitakapopewa ridhaa ya kubeba bendera ya CCM katika nafasi
ya Urais na pia nitakapopewa ridhaa ya kuliongoza Taifa letu kupitia uchaguzi
mkuu wa mwaka huu.
Ramani ya Uongozi Imara Ninaouamini 9
Leadership Roadmap)
Kama
nilivyotangulia kusema, kazi ya kuongoza nchi si lelemama na hasa unapoongozwa
na dhamira ya dhati na msukumo wa ndani ya nafsi unaojielekeza kubadilisha
maisha ya wananchi wenzako waliokuamini uwaongoze. Kwa vyovyote vile, hiyo
haiwezi kuwa kazi ya mtu mmoja. Ni kazi ya pamoja.
Lakini
ili muweze kufanya kazi kama timu moja iliyojipanga kisawasawa kuleta
mabadiliko yanayohitajika na ili muweze kweli kutoa Uongozi imara unaojikita
kujenga Taifa imara hapana budi kiongozi mkuu anayeongoza timu hiyo aweke
ramani anayokusudia kuifuata katika kutoa uongoziimara anaoukusudia yaani
‘Leadership Roadmap’.
Pamoja
na kuwa sehemu ya uongozi huko nyuma, kutakuwa na maamuzi na matumaini mapya.
Ramani ya uongozi imaraninayokusudia kuutoa kwa wenzangu na ambayo nitaitumia
kuiongoza timu yangu katika kuwatumikia Watanzania wenzangu itajikita katika
maeneo yafuatayo:
1.
Kurejea kwenye Katiba katika kuainisha nia, dhamira na malengo yetu ya kujenga
jamii inayozingatia misingi ya demokrasia, udugu na amani. Muhimu katika hili
ni kukemea tabia mbaya zinazochochea mfarakano katika jamii kama vile matumizi
mabaya ya siasa za udini na ukabila.
Aidha
moja ya misingi muhimu ya Katiba ni Muungano wetu. Itakuwa dhamira yangu
kuimarisha misingi ya Muungano pamoja na udugu wa damu nahistoria ya
ushirikiano iliyojengwa na waasisi wetu, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Hayati Sheikh Amri Abeid Karume na kuyaenzi Mapinduzi matukufu ya
Zanzibar.
2.
Kujenga fikra mpya za kurejesha kujiamini na kufufua azma ya kujitegemea kama
Taifa. Ni dhahiri kuwa pamoja na rasilimali zetu, bado Tanzania ni taifa
tegemezi. Bado tunajidanganya kuwa wafadhili watatujengea nchi. Tukumbuke, nchi
zinajengwa nawananchi wake.
Nasi
pia lazima tujikomboe kifkra na tuondokane na utamaduni wa kuwa tegemezi.
Tuanze kwa kujipiga kifua kwa kujiamini kuwa tunaweza kujitegemea na kuijenga
Tanzania sisi wenyewe.Kujiamini na kujitegemea ndio uhuru wa kweli.
3.
Kujenga uzalendo, uadilifu ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwazi katika shughuli
zote za serikali na kupambana na rushwa.Watanzania tumepoteza uzalendo kwa
kiasi kikubwa. Kuna vitendo vinavyoashiria kuwa hatuipendi tena nchi
yetu.
Tunashabikia
wizi na rushwa. Inabidi turejee kwenye misingi ya taifa letu misingi ya
uadilifu na uzalendo. Tukumbuke kuwa hatuwezi kujenga uchumi wa kisasa kama
tutaruhusu rushwa ishamiri.
Wawekezaji
hawataleta mitaji yao kwa wingi kama rushwa itaendelea kutawala katika huduma
serikali na wananchi hawawezi kupata huduma bora kama rushwa itaendelea
kutawala. Ni lazima tuipinge rushwa kwa vitendo sio maneno.
4.
Kujenga Serikali madhubuti, makini na yenye nidhamu inayoendeshwa kwa misingi
ya sheria, uwazi na uwajibikaji.Maendeleo ya watu hayawezekani bila serikali
kusimamiautekelezaji sera na miradi na kuleta ufanisi katika kutoa huduma na
kusimamia maendeleo. Tumekuwa wepesi wa kutunga sera lakini wazito wa
kuzitekeleza na kuzisimamia.
5.
Kuleta msukumo mpya wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika
ujenzi wa uchumi wa kisasa na unaojitegemea. Sekta binafsi ndiyo nyenzo ya
uchumi imara. Inazalisha mali, ajira na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato
la taifa kwa kulipa kodi.
Ilisekta
hii itoe mchango unaotakiwa katika maendeleo ni lazima ifanye kazi na serikali
kwa karibu. Tukumbuke, bila uchumi imarahakuna huduma bora!
6.
Uwekezaji katika huduma za jamii. Elimu na afya bora, mazingira, makazi safi na
maji salama ndiyo mihimili ya maendeleo ya watu.
Hii
inawezekana tu iwapo serikali itakuwa na sera na utashi wa kuutambua uboreshaji
wa huduma za jamii kama ndiyo lengo kuu la maendeleo ya nchi. Serikali
nitayoiongoza itahakikisha kuwa kila Mtanzania anapata elimu bora na
inayogharamiwa na serikali kama mimi na wenzangu tulivyopata.
Wakatitunazungumzia
kuunganisha soko la ajira katika Afrika Mashariki, hatuna budi kurekebisha
mfumo wetu wa elimu na kuuelekeza kwenye mafunzo ya ufundi na ustadi
yanayowajenga wahitimu wetu kuwa wabunifu, wenye kujiamini, wenye uwezo
kushindana katika soko la ajira na wa kujiajiri. Napenda kusisitiza kuwa elimu
ndiyo muhimili wa maendeleo, ndiyo mkombozi wa kweli wa binadamu. Mimi ni mfano
hai wa ukombozi wa elimu.
Elimu
ndiyoimenivusha kutoka kijijini kwetu Ngarash na kunipa upeo wa kitaifa. Mama
akiwa na elimu atajua umuhimu wa kumpeleka mwanae shule, anapata lishe bora na
chanjo stahili na kuwa anaishi katika mazingira safi. Elimu ndilo jibu la
umaskini, maradhi na ujinga.Taifa lililo elimika ni taifa lenye maendeleo.
7.
Kujenga uchumi shirikishi unaolenga kuondoa umaskini.Mkakati wa kuondoa
umaskini Tanzania lazima ujikite kwenye nguzo za ushiriki wa kila Mtanzania
katika uchumi wa taifa.
Kwa
misingi hii, tukiweza kupunguza umaskini, tutaweza pia kupunguzatofauti za
kipato ambazo tukiziacha ziendelee kukua kwa kiasi cha sasa, zinaweza
kuhatarisha utulivu na amani katika jamii yetu.Uchumi shirikishi ndio silaha
dhidi ya umaskini.
8.
Kuimarisha ulinzi wa nchi na usalama wa raia na ujirani mwema.Itakuwa nia yangu
kuimarisha misingi iliyojengwa kulinda na kudumisha umoja na amani
nchini.
Kadhalika,
nitahakikisha kuwa usalama wa mipaka ya Tanzania unaimarishwa kwa misingi ya
ujirani mwema na kutanzua migogoro na matatatizo yoyote na nchi jirani, kwa
njia ya diplomasia na mazungumzo.
Hitimisho:
Hii
ndiyo misingi na dira ya uongozi wangu. Nachelea kusema kuwa haitakuwa kazi
rahisi. Lakini kwa ushirikiano wa kila mmoja na maamuzi magumu, yote
yanawezekana.
Tumeona
nchi nyingi zilizosimamiwa na utawala thabiti wa serikali za kimaendeleo
zikikabili na kupunguza umaskini katika kizazi kimoja. Kama mataifa mengine
yamefanikiwa, tena bila raslimali kama zetu, kwa nini sisi tushindwe?
Tuna
kila sababu ya kufanya maamuzi magumu sasa ili kuwajengea Watanzania matumaini
mapya ya maendeleo. Naomba nisisitize kuwa katika uongozi wangu hakutakuwa na
nafasi ya majungu, na visasi. Hatutaangalia nyuma bali tutasonga mbele kwani
ndicho Watanzania wanakitarajiakutoka kwa uongozi uliojengwa kwenye misingi
bora.
Ndugu Watanzania:-
Ni
maono yangu kuwa siku si nyingi nchi yetu itaanza safari yenye uelekeo wa
matumaini na neema tele kwa wananchi.
Ni
maono yangu kuwa siku si nyingi sisi kama Watanzania kwa umoja wetu tutajivunia
kuishi katika nchi tunayoipenda na inayoendeshwa kwa misingi ya utawala bora,
chini ya serikali ya kimaendeleo iliyojengwa kwenye fikra mpya za uzalendo,
uadilifu, utendaji na uwajibikaji.
Ni
maono yangu kuwa Peke yangu sitaweza, lakini kwa maamuzi magumu na ushirikiano
wa kila mmoja wetu ikiwa ni pamoja na wagombea wenzangu ndani ya CCM,
inawezekana kuanza safari hii ya Matumaini Mapya.
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu hii fupi, kuna mambo matatu ningependa kuyaweka wazi
hapa.
La
kwanza, linahusu msingi wa uongozi ninaouamini na ambao nimeusema mara kadhaa
hapa. Msingi huo ni UWAJIBIKAJI.Watanzania wananifahamu mimi si mtu wa maneno,
ni mtu wa vitendo. Naamini kwa dhati kabisa kwamba huwezi kuwa na Uongozi imara
utakaoweza kusimamia ujenzi wa Taifa imara iwapo huna ujasiri wa kuwajibika.
Mimi nimeongoza kwa mfano, na pale ilipobidi, nilikubali kuwajibika na kubeba
dhamana ya uongozinilipojiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu.
La
pili, mimi si mtu wa visasi. Siamini katika kuangalia ya nyuma. Yaliyopita si
ndwele, tugange yajayo. Na kwa nini tuangalie nyuma wakati kama taifa tuna kazi
kubwa sana mbele yetu inayohitaji kufanywa? Mimi ni Mkristo; najifunza kutoka
kwa Bwana Yesu ambaye alipoulizwa: “Nisamehe mara ngapi?” Alijibu, “Samehe mara
sabini mara saba”. Nitaenzi na kudumisha utamaduni huu wenye sura ya utu na
heshima.
La
Tatu, natambua kwamba dhamana ya Urais ni shughuli nzito hasa kwa taifa ambalo
lina changamoto nyingi. Nataka niwahakikishie Watanzania wenzangu kwamba afya
yangu ni njema kuweza kuwatumikia katika jukumu hili zito. Pamoja na vijineno
vinavyosemwa pembeni, mimi mwenyewe ndiye ninayejijua zaidi. Nawahakikishia
kuwa nisingekuja hapa leo na kueleza nia yangu hii ingekuwa sina uhakika na
afya yangu.
Natoa
RAI kwa Chama changu cha CCM, nadhani umefika wakati kwamba tutende tofauti na
mazoea, watu wote walionyesha nia ya kutaka kuongoza, liundwe jopo la madaktari
wa ndani na nje ya nchi tupimwe afya zetu, kwa hili najitolea kuwa wa KWANZA
KUPIMWA afya yangu
Safari
tuianze leo, hatuna kesho nyingine.
Ahsanteni
sana kwa kunisikiliza
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni