Marafiki zangu, ndugu zangu, watanzania wenzangu, salaam! Kwa muda mrefu, na kwa njia mbalimbali za mawasiliano, mmekuwa mkinidadisi mbona kimya kuhusu mwaka 2015? Pamoja na kwamba mara nyingi mlitaja mwaka tu, lakini niliwaelewa. Wengi mliushangaa ukimya wangu.
Pamoja kwamba ukimya ni haiba yangu na ni karama aliyonitunuku Mwenyezi Mungu, Muweza wa yote, baadhi yenu niliwajibu 'Ukimya Una Kishindo'! Sina uhakika kama yafuatayo ni kishindo, lakini ni taarifa rasmi kutoka kwangu.
Kwa staili ya siku hizi tunajitokeza na kutamka: tutatangaza nia siku hii au ile. Kwa kusema hivyo tayari tumetangaza nia! Basi nami kwa staili hiyo hiyo nawataarifu kwamba, majaaliwa, natarajia kutangaza nia ya kuomba ridhaa ya wanaCCM wenzangu wanichague ili niwe mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Natarajia kutangaza nia hiyo Jijini Mbeya, jumatatu, tarehe 1, saa 4 asubuhi, katika ukumbi wa mikutano wa CCM Mkoa wa Mbeya.
Wale mtakaoweza kufika karibuni, na ninyi ambao hamtaweza kufika basi tutakiane heri.
Kubwa zaidi Mwenyezi Mungu atujalie kwa yote na rehema zake nyingi ziwe juu ya nchi yetu. Mungu ibariki Tanzania.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni