Alhamisi, 28 Mei 2015

LEO NI MIAKA MIWILI IMEPITA TANGU ALBERT MANGWAIR AFARIKI DUNIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete aliwahi kusema anasikitika kuona kwamba zamani watoto walikuwa wakiwazika wazazi wao, lakini katika maisha ya sasa wazazi wamekuwa wakiwazika watoto wao. Ni kweli, na ni jambo la kusikitisha lakini kama wasemavyo, afanyalo Mungu halina makosa

Leo ni miaka miwili tangu rapper Albert Mangwea afariki dunia. Habari kuhusu kifo chake, zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuenea kwa kasi mitaani. Zilikuwa kama uvumi tu na wengi walihisi ni utani ambao baadaye ungeisha lakini ikaja kubainika kuwa ni habari ya kweli.

Ilikuja kufahamika kuwa Ngwair akiwa na rafiki yake M TO THE P waliopelekwa kwenye hospitali ya St Helen ya jijini Johannesburg wakiwa mahututi. Mpaka leo haijulikani kipi kiliwakuta. 

Utata huo ulisababisha wengi kuanza kuvumisha kuwa wasanii hao walikuwa wametokea kutumia kiasi kikubwa cha madawa ya kulevya. Marafiki waliokuwa wakilala chumba kimoja na Ngwair walidai kuwa mpaka anapelekwa hospitali alikuwa hajitambui na huenda alifariki akiwa usingizini. Taarifa za kifo cha Ngwair ziliitikisa Tanzania. Radio zikasikika zikipiga nyimbo zake muda mwingi na kufanya vipindi maalum. 

Kifo cha Ngwair kilisababisha wasanii wengi kuahirisha mipango yao ikiwa ni pamoja na kusogezwa mbele kwa show za Mwana FA, Lady Jaydee, Izzo B na zingine. 

Katika kipindi hicho wasanii walisitisha kutoa nyimbo ama video zao kwa heshima yake. “Inaniuma sana lakini sina cha kufanya kwa kuwa ni kazi ya Mungu na kazi yake haina makosa, kinachotakiwa ni kumuombea apumzike kwa amani huko aendako,”alisema Profesa Jay. 

“Sidhani kama atanitoka kichwani kwangu, naona kama ametutoroka kwa kuwa hatuhitaji aondoke muda huu lakini hakuna jinsi tutakutana naye siku ya mwisho na nitamweleza machungu yangu na kwa jinsi gani kifo chake kimeniumiza,” alisema Afande Sele. Kipaji cha Albert Mangwea katika uandishi wa mashairi ya hip hop na uwezo wa kufanya mitindo huru haukuwa na mfano na bado alikuwa na mustakabali mzuri kimuziki. 

Ngwair ni miongoni mwa wasanii wa hip hop waliokuwa na hits nyingi na wenye mashabiki wengi. Hiyo ilidhihirika siku mwili wake unapokelewa uwanjani, siku mwili wake unaagwa kwenye uwanja wa Leaders jijini Dar es Salaam na siku anazikwa mjini Morogoro. Tanzania ilipoteza jembe. Mangwair alizikwa June 6 kwao Morogoro. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni