Alhamisi, 28 Mei 2015

"ALBINO HAWEZI KUKUPA UBUNGE" ADAI WAZIRI SILIMA

WANASIASA wameambiwa kuwa ubunge hautatokana na kiungo cha albino na kuachana na fikra hizo potofu.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Perreira Ame Silima amekiri bungeni kuwa ni kweli zipo taarifa kuwa baadhi ya wanasiasa wanahusishwa na imani potofu za kutumia viungo vya binadamu ili kupata madaraka.

"Ni kweli habari ziko zinazungumzwa kuwa wanasiasa fulani na zinaibuka wakati kama huu ambako kuna joto kali la Uchaguzi Mkuu," alisema Silima na kuongeza: "Ubunge hautatokana na kiungo cha albino."

Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CCM), aliyesema vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vinaeleza kuwa wapo wanasiasa wanaotumia viungo vya albino kusaka umaarufu.

"Vyombo hivi vya habari vya ndani na nje ya nchi vinaeleza kuwa wapo wanasiasa waokwenda kwa waganga na kutumia viungo vya albino kujitafutia umaarufu. Kwa nini serikali isiwabane waandishi hawa ili iwataje wanasiasa hao ili wasiohusika wasitiwe doa," alihoji mbunge huyo wa Rombo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani alisema serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa katika kukabiliana na tatizo la mauaji ya watu wenye ulemavu, na kuwa lazima jamii kuanzia ngazi ya familia ibadili fikra zao.

Alisema haiwezekani albino wauawe katika baadhi ya mikoa au eneo fulani tu la nchi, hivyo elimu inahitajika kwa watu husika na kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua zikiwamo za kuielimisha jamii.

Aidha, alisema kifaa maalumu kitakachofungwa kwa albino ili kufuatilia mienendo yao, kinaendelea kufanyiwa kazi na serikali ili kufahamu kama teknolojia kinafanya kazi na pia kufahamu kama ni salama.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama, alisema serikali haijalidanganya Bunge kuhusu kifaa hicho, na kuwataka wabunge kuungana pamoja na serikali katika kukomesha mauaji hayo yanayolitia aibu Taifa.

Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Philipa Mturano (Chadema), Silima alisema mpaka sasa watu 15 wa mauaji ya albino, wamekamatwa, kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.(HABARI LEO)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni