Alhamisi, 12 Machi 2015

LUKUVI AIBUA UVUNDO ILEMELA

William Lukuvi: Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Mwanza. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amebaini madudu yanayofanywa na Idara ya Ardhi Mkoa wa Mwanza na kusema kuwa, mkoa huo una utaratibu mbovu wa upimaji na utoaji hati za viwanja.
Pia, Lukuvi jana alilazimika kutoa Sh1 milioni baada ya Baraza la Ardhi la mkoa huo kukosa Sh40,000 ya kununulia karatasi za kuandikia hukumu kwa kesi 35.
Hayo yalibainika kwenye ziara yake mkoani hapa, baada ya kutembelea baraza hilo na kuzungumza na wananchi wa Ilemela.
Wananchi hao walimweleza waziri huyo kuwa, watumishi wa idara hiyo wamekuwa kama miungu watu, kwani wamejimilikisha ardhi sambamba na kugawa viwanja vngine kwa wenye fedha katika maeneo wanayomiliki kihalali.
Baadhi ya watumishi wa idara hiyo waliotuhumiwa kupora ardhi ni ofisa ardhi mkoa na ofisa ardhi wa Manispaa ya Ilemela (majina yanahifadhiwa).
Katika mkutano huo, Shida Lukanda alisema idara hiyo ndiyo yenye matatizo, yanayosababisha wananchi wakikosa haki zao.
“Waziri, Mwanza tuna matatizo makubwa kwenye suala la ardhi, tunadhulumiwa viwanja vyetu, tunaporwa,” alisema Lukanda.
Alipowasili Lukuvi alipokea nakala za malalamiko lukuki kutoka kwa wananchi waliofurika kutoa malalamiko yao na ushahidi wa vielelezo mbalimbali.
Wakati huohuo, liliibuka suala la ujenzi wa Zahanati ya Bwiru, wananchi walidai kuporwa eneo lao na Manispaa ya Ilemela na kujenga nyumba za watumishi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo aliingilia kati na kutaka ukweli kuhusu eneo hilo, kwani kabla ya kujenga nyumba za watumishi walitakiwa kuwaeleza wananchi hali halisi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni