Lilian Internet
Mnenguaji mahiri na mkongwe nchini, Lilian Internet(35), amesema vijana wengi walio katika fani hiyo wanajihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.
Nyota huyo, mzaliwa wa Mkoa Kilimanjaro, pia amelaani tabia ya baadhi ya vijana kuwa na wapenzi wengi huku akisema anamshukuru Mungu kwa kuwa ameweza kujiepusha na tabia hiyo na sasa ni mke wa mtu.
“Asilimia kubwa ya wanenguaji wanatumia dawa za kulevya, si kwa sababu wanatumia dawa hizo ili wacheze vizuri jukwaaani, bali waliingia huko kwa kufuata mkumbo. Jambo hilo silifurahii linaniumiza sana,” anasema Internet.
Mnenguaji huyo ambaye jina lake halisi ni Lilian Josephat Tungaraza anasema tatizo hilo ni kubwa na vijana wengi, hasa wasichana wameangukia katika tabia hiyo kwa kudanganywa na wanaume na wakati mwingine wao wenyewe kuwa watapata nguvu zaidi za kucheza jukwaani.
“Mimi nafanya vizuri na mashabiki wengi wanafurahia kazi yangu tangu nilipojiunga na Bendi ya Twanga Pepeta mwaka 1997 ilipoanza. Mpaka leo wengi wakiniona wanadhani nina miaka 20, lakini hii yote inatokana na kujali afya yangu. Naomba Mungu awajalie ili watokane kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwani wengi wanadhalilika, hiyo inaniumiza,” anasema.
Lilian anasema mama yake ambaye ni mwenyeji wa Mwanga mkoani Kilimanjaro, amekuwa na mchango mkubwa katika maisha yake kutokana na kumuunga mkono kwa kazi anayoifanya, hivyo kusaidia kuwa naye karibu katika mambo mbalimbali.
“Wakati wa kwenda kazini, kuna vyakula ninavyotakiwa kula ambavyo sivitumii sana. Sina ulevi ninaotumia zaidi ya bia mbili kwa siku. Vilevi vilivyokatazwa mimi situmii,” anasema.
Msanii huyo anaeleza kuwa hunywa baada ya kazi au wakati mwingine akiwa nyumbani siku ya Jumatatu ambayo ni mapumziko kwake.
Akizungumzia mafanikio yake anasema: “Ni kujitunza kwa sababu hii ni kazi ngumu. Kuna vitu unatakiwa kuwa unavifahamu na kutekeleza; kwanza ni kulala mapema, kuwa na kiasi katika utumiaji wa pombe, lakini pia kutokuwa na wanaume wengi kwani hiyo inakufanya pia upoteze mwelekeo.”
Kauli hiyo inaungwa mkono na Mkurugenzi wa Twanga Pepeta International Asha Baraka anayesema: “Tumeona wasanii wengi wa Tanzania ambao awali walikuwa wanafanya vizuri, lakini baada ya kujaa sifa na kukutana na marafiki wengi hasa makundi, wakazama kwenye dawa za kulevya, sasa wanatapatapa na kubaki kulaumu, wakati wenyewe wamejiharibia.”
Hata hivyo, Asha anasema Twanga Pepeta imekuwa ikitoa mafunzo kwa wasanii ili kujiweka kando na matumizi ya dawa za kulevya kupitia vikao vyao wakiwataka pia kuwa na nidhamu ya kazi.
“Nidhamu ya kazi ni jambo linaloingia katika haya yote. Nimekuwa nikiwaashauri wasanii wangu katika haya na mara nyingi tumefanya hivyo ndiyo maana unaona Twanga Pepeta imesimama mpaka leo, mengine yanatokana na msanii mwenyewe kujibana katika makundi yasiyofaa,” anasema Asha Baraka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni