Na Chibura Makorongo, Simiyu
ASKARI wa Jeshi la Polisi na Magereza, wametiwa mbaroni kwa kukutwa na noti bandia pamoja na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Askari hao ni Konstebo Seleman Juma (25) wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Simiyu na Edmund Masaga (28), ambaye ni askari Magereza wilayani Bariadi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, alisema askari hao walitiwa mbaroni juzi saa 9:00 alasiri katika mtaa wa Old Maswa wilayani Bariadi.
Alisema askari hao walifika katika kibanda cha kutolea fedha kinachomilikiwa na Mwalimu wa Sekondari ya Old Maswa, Kassian Luhende (29), kwa lengo la kuweka fedha.
Alisema baada ya Luhende kupokea fedha sh. sh. 100,000, alizitilia shaka na kubaini si halali na kuomba msaada kwa wafanyabiashara wenzake na kuwakamata watuhumiwa hao.
Hata hivyo, katika mahojiano baada ya kukamatwa, mmoja alitoa kitambulisho cha kazi na kubainika kuwa ni askari na mwingine alidai ni dereva wa bodaboda.
Kamanda Mkumbo alisema katika kuwapekua watuhumiwa hao, PC Juma alinaswa na noti bandia zingine zenye thamani ya sh. milioni 1.9. Pia, alikutwa na sare za JWTZ.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni