Alhamisi, 5 Februari 2015

JK: Sakata la gazeti la The EastAfrican linashughulikwa


Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck, akiongozana na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete, akisalimia wakazi wa jijini, Dar es Salaam alipowasili kwenye Viwanja vya  Ikulu, Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame 

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema suala la kupigwa marufuku kusambazwa kwa gazeti la The EastAfrican Tanzania, linafanyiwa kazi na taratibu zote zikikamilika, litaruhusiwa.
Wiki mbili zilizopita gazeti hilo linalomilikiwa na Kampuni ya Nation Media Group, lilipigwa marufuku kusambazwa nchini, ikiwa ni miaka 20 tangu kuanzishwa kwake kwa ajili ya kuandika habari za ukanda wa Afrika Mashariki.
Uamuzi wa kulifungia gazeti hilo ulichukuliwa kjwa kile kilichoelezwa kuwa limekuwa likisambazwa nchini bila ya kuwa na usajili, kinyume na Kifungu cha 6 cha Sheria ya Magazeti, Namba 3 ya mwaka 1976.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Ikulu Dar es Salaam, akiwa pamoja na Rais wa Ujerumani Joachim Gauck, ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tano.
Rais Kikwete alikuwa akijibu swali lililoulizwa na mmoja wa wanahabari walioambatana na Rais Gauck, ambaye pamoja na mambo mengine alitaka kujua ni lini gazeti hilo litafunguliwa na sababu za kupigwa marufuku.
Rais Kikwete alisema: “Lilikuwa na matatizo ya usajili, sasa wameanza kufanya maombi na suala lao linashughulikiwa, taratibu zikikamilika litaruhusiwa kusambazwa nchini.
Aliongeza: “Nchi hii ina magazeti mengi, lakini ya Serikali ni mawili tu... moja linaandika kwa lugha ya Kiswahili na jingine Kiingereza (Habari Leo na Daily News). Yapo magazeti kama Mwananchi, Tanzania Daima, The Guardian, Nipashe, Majira na mengine mengi tu.”
Alisema Serikali inazingatia uhuru wa vyombo vya habari, lakini pia iko makini kuhakikisha vyombo hivyo vinafuata sheria na taratibu zilizowekwa.
“Barua ya Januari 21, 2015 iliagiza kusimamishwa mara moja kwa uchapishaji na usambazaji wa gazeti hilo Tanzania hadi litakaposajiliwa rasmi na Msajili wa Magazeti, Idara ya Habari,” alisema.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni