Alhamisi, 5 Februari 2015

Ivory Coast yatinga fainali Afcon


Kiungo wa Ivory Coast, Yaya Toure (kulia) akishangilia na wenzake baada ya kufunga bao la kwanza kwa timu yake dhidi ya DR Congo wakati wa mchezo wa nusu fainali ya Mataifa ya Afrika iliyofanyika usiku wa kumkia leo kwenye Uwanja wa Bata. Ivory Coast ilishinda 3-1. Picha na AFP 

Malabo, Guinea ya Ikweta.
 Ivory Coast imefuzu kucheza Fainali ya Mataifa ya Afrika baada ya kuichapa DR Congo kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Bata.
Ivory Coast ilipata mabao yake kupitia Yaya Toure, Gervinho na Wilfried Kanon wakati bao la kufutia machozi la DR Congo lilifungwa na Dieumerci Mbokani kwa mkwaju wa penalti.
Ivory Coast imefuzu kwa fainali mara tatu tangu 2006, lakini imeshindwa kunyakuwa ubingwa ikifungwa na Misri (2006) na Zambia 2012.
Yaya alifunga bao la kwanza kwa Tembo hao dakika 21, akiunganisha mpira uliopigwa vibaya na Bony, lakini bao hilo lilidumu kwa dakika mbili kabla ya Mbokani kusawazisha kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Ivory Coast kushika mpira kwenye eneo la hatari.
Uzembe wa mabeki wa Congo ulitoa mwanya kwa mshambuliaji mpya wa Manchester City, Bony kutengeneza pasi kwa Gervinho ambaye hakufanya ajizi akiwa katika eneo la 18 na kupiga shuti lililomshinda kipa Robert Kidiaba na kujaa wavuni dakika 41. Kabla ya Kanon kupachika bao la tatu dakika 67 akiunganisha kwa goti mpira wa kona.
Ivory Coast sasa inasubiri mshindi wa leo kati ya wenyeji Equatoria Guinea dhidi ya Ghana.
Timu hizo mbili ni kama zipo kwenye anga tofauti, ingawa zitakuwa chini ya uongozi wa wachezaji wazoefu, Asamoah Gyan (Ghana) anayecheza soka ya kulipwa Falme za Kiarabu (UAE) na Emilio Nsue wa Guinea ya Ikweta anayecheza soka kwenye klabu ya Ligi Daraja la Kwanza, England, Middlesbrough.
Hata hivyo, Ghana au Black Stars ambayo imetwaa mataji manne ya fainali hizo inapewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo wa leo.
Huo, utakuwa ni mchezo unaokutanisha wababe wa soka la Afrika, Ghana wanaoshika nafasi ya 31 kwenye msimamo wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), dhidi ya wenyeji wanaoshika nafasi ya 81 duniani.
Kivutio pekee kitakuwa ni kwa washambuliaji wa Ghana kuzima ngebe wa wenyeji Guinea ya Ikweta ambao hawajafungwa mechi yoyote kwenye fainali za mwaka huu.
Ikilinganishwa na Ghana, Guinea ya Ikweta inaonekana ipo vizuri zaidi, ikiwa na bahati kama ile ya robo fainali walipoiduwaza Tunisia kwa mabao 2-1.
Kwa upande wao, Ghana walianza fainali hizo kwa kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Senegal kwenye mechi ya ufunguzi na kufuatiwa na ushindi kwenye mechi tatu zilizofuata, ikiwamo ya robo fainali walipoilaza Guinea kwa mabao 3-0
.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni