Jumatatu, 12 Januari 2015

Vyama vya michezo vilivyojipanga 2015

Leo ni siku ya 12 tangu kuanza kwa mwaka mpya wa 2015 ambao wanamichezo wengi wanatarajia utakuwa mwaka wa mabadiliko katika usimamiaji wa michezo mbalimbali nchini.
Mwaka uliopita Tanzania ilifanya vibaya kwenye mashindano ya kimataifa, hali ambayo imevishtua vyama vya michezo na hivyo viongozi wa vyama hivyo kuamua kuweka mikakati kwa ajili ya usimamizi mzuri mwaka 2015.
Spoti Mikiki limezungumza na viongozi mbalimbali wa vyama vya michezo ili kubaini mikakati yao na namna gani wamejipanga kuondoa ukame wa medali kwa taifa mwaka huu.
Shirikisho la Riadha (RT)
“Tunachokihitaji ni kupata shule maalumu ambayo wanariadha watasoma na sisi RT kupeleka makocha wetu ambao watakuwa wakitoa programu maalumu ya riadha shuleni hapo,” anasema Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui.
Anasema hakuna kinachoshindikana na watapata sapoti hiyo na uwezeshwaji kutoka kwa wadau kwani 2014 waliweka mkakati kama huo na kufanikiwa kuteua vijana 40 katika mashindano ya Umisseta na Umitashumta.
“Kikubwa tupate shule moja ambayo itatoa fursa kwa wanariadha wetu kusoma na kufanya mazoezi, huo ndiyo mkakati tuliouona mwaka huu, tunahitaji kuwa na wanariadha wengi vijana ambao wataanza kuandaliwa kwa michezo ya Olimpiki,” alisema.
Nyambui alisema tayari wameandaa kalenda yao ya mwaka huu na kufafanua kuwa wanaandaa mpango mkakati wa maendeleo ambao utawasaidia kupata udhamini kwa wadau ili kufanikisha malengo yao ya 2015.
Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT)
Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga anasema watautumia mwaka huu kurejesha hadhi ya masumbwi nchini, kwa kuanzia watawapeleka makocha wao kusoma ili wawe na utaalamu wa kimataifa.
“Tukiwa na makocha wenye ujuzi ni wazi timu ya taifa itakuwa na ujuzi pia, lakini tunachokiangalia mwaka huu ni kuwa na timu imara ya vijana itakayoandaliwa kwa muda mrefu zaidi ili kupata mabondia wenye hali, uwezo na nguvu ya ushindani.
“Mwaka uliopita hatukuwa na mawasiliano mazuri na wadhamini, hali hiyo pia ilitugharimu katika malengo yetu, lakini kwa kushirikiana na Serikali tumeweka mikakati ili kuwa na udhamini wa kudumu na kuihudumia timu yetu ipasavyo, pia Watanzania watuunge mkono katika mpango huu ili kurejesha hadhi ya ngumi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,” anasema Mashaga.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni