Jumapili, 11 Januari 2015

CCM Yatangaza vita

SHARE THIS
TAGS
nnauyeCHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kufanya maandalizi ya kupigana na wafuasi wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kinaowatuhumu kuwashambulia wanachama wake.
Kimesema uamuzi huo umekuja baada ya kuchoshwa na vurugu zinazofanywa na wafuasi wa Ukawa katika maeneo mbalimbali hapa nchini hususan wakati wa kutangaza matokeo na uapishaji wa viongozi wa Serikali za Mitaa.
Mpango huo wa mapambano umetangazwa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu msimamo wa chama chake dhidi ya vurugu za kisiasa zinazotokea sasa katika baadhi ya maeneo nchini.
“CCM kinalaani vikali vurugu zilizofanywa na wafuasi wa Chadema na CUF kwa viongozi wetu wa Serikali za mitaa katika maeneo kadhaa nchini, vurugu hizo licha ya kuharibu utaratibu wa kuapisha pia zilisababisha baadhi ya viongozi wetu kujeruhiwa, sasa tunasema imetosha uvumilivu umefika mwisho.
“Endapo mamlaka husika hazitokuwa tayari kuwadhibiti vijana wanaojihusisha na vurugu hizo, chama kipo tayari kuchukua hatua za kukabiliana na watu hao,” alisema Nape.
Alisema vurugu zinazofanywa ni muendelezo wa tabia ya mazoea ya vyama vya upinzani nchini kutoheshimu sheria na taratibu za nchi.
Nape aliwataka wanachama na wafuasi wa vyama vya upinzani kukubali uamuzi unaotolewa na wananchi katika chaguzi badala ya kupinga kwa fujo.
“Wapinzani wanapaswa wajipange kutatua upungufu wao badala ya kufanya vurugu, utaratibu wa kufanya vurugu haupo sawa na haukubaliki kama kuna taratibu zimekiukwa na wasimamizi kwa mapenzi na utashi wao, kwa kuzidiwa na ubinadamu zipo taratibu za kufuata kama kwenda mahakamani,” alisema Nape.
Alisema iwapo malalamiko ya wapinzani ni kubadilishiwa matokeo, hata CCM kuna maeneo ambayo wamepata matatizo kama hayo lakini wahusika wameshauriwa kwenda mahakamani badala ya kufanya vurugu.
Wakati huo huo, Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, leo inatarajia kukutana jijini Dar es Salaam kwa siku moja katika kikao cha maandalizi ya kikao cha Kamati Kuu kitakachofanyika Ofisi za Makao Makuu ya chama, Zanzibar Januari 13.
Kwa mujibu wa Nape, kikao cha sekretarieti ambacho kitaongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, kitaandaa ajenda za Kamati Kuu itakayoongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Jakaya Kikwete.
“Baada ya sherehe za Mapinduzi, Kamati Kuu ya Taifa itakutana Zanzibar Januari 13, kikao kitakuwa ni cha kawaida cha siku moja chini ya Mwenyekiti wa CCM,” alisema Nape.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni