Moja ya nyumba zilizoteketezwa katika
Kijiji cha Murufiti ambapo watu saba waliuawa kwa kuchomwa moto. Picha na Diana
Rubanguka.
Na Diana
Rubanguka na Antony Kayanda, Mwananchi
Kigoma. Watu saba wameuawa kwa kuchomwa
moto ndani ya nyumba katika tukio ambalo nyumba 18 ziliteketezwa na mbili
kubomolewa na wananchi waliodai wanawaua wachawi katika Kijiji cha Murufiti,
Kasulu, mkoani Kigoma.
Miongoni mwa waliouawa katika tukio
hilo lililotokea Jumatatu iliyopita ni John Mavumba (68) na mkewe Elizabeth
Kaje 55 ambao pamoja na wenzao walikuwa wakituhumiwa kuwa ni washirikina.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi, Josephat John ambaye ni mtoto wa Mavumba, alisema wazazi wake walichomwa
moto na kundi la vijana waliokuwa wakiwatuhumu kuwa ni wachawi.
Alisema vijana walikuwa wamebeba
mapanga, marungu na kupita katika nyumba mbalimbali wakifanya mauaji wakisema
maneno kwa kurudiarudia kwamba watawamaliza wachawi kwa kuwaua, ndipo yeye na
wenzake walikimbia usiku huo wakihofia kuuawa.
“Niliporudi alfajiri niliukuta mwili
wa mama ukiwa umbali wa mita 10 kutoka ilipo nyumba yetu ukiwa umeungua na
mwili wa baba ukiwa umeungua ndani ya nyumba,” alisema John.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma,
Jafari Mohamed alisema mauaji hayo yalitokea Oktoba 6 kuanzia saa 4:00 usiku
katika kijiji hicho.
John alisema baada ya tukio hilo
wanaume wengi wameyakimbia makazi yao wakihofia kuuawa na kundi la vijana hao.
“Kijiji kimebaki na wanawake tu, wanaume wamezikimbia nyumba zao wanahofia
kuuawa,” alisema.
Mohamed alisema mauaji hayo
yametokana na imani za kishirikina.
Aliwataja waliouawa kuwa ni John
Muvumba (68), Elizabeth Kaje (55), Dyaba Kitwe (55), Vincent Ntiyaba (42),
Herman Ndabiloye (78), Redempta Mdogo (60) na Ramadhan Kalaliza (70) wote
wakazi wa kijiji hicho.
Alisema nyumba zilizochomwa moto ni
18, mbili zilibomolewa na kufanya jumla ya nyumba 20 zilizoharibika kabisa.
Wakazi wa kijiji hicho, Zablon Andrew
na Eveline Enock walisema kwa nyakati tofauti kuwa chanzo cha mauaji hayo ni
mganga wa jadi aliyefika kijijini hapo na kupiga ramli akiwataja watu waliouawa
kuwa ni wachawi.
Andrew alisema baada ya mganga huyo
kuwataja, vijana walikusanyana na kuanza kuwateketeza watu bila huruma.
“Kitendo hiki kimeturudisha nyuma
kimaendeleo kwa sababu nyumba zetu zimechomwa moto na mazao yetu yameharibiwa,”
alisema Andrew.
Hali ilivyo kijijini
Mmoja wa watu aliyechomewa nyumba,
Evelyne Msilu alisema sasa kijiji hicho kina askari wengi wanaofanya doria.
“Hali inasikitisha, tumepoteza ndugu
zetu waliouawa, wanaume wengi wamekikimbia kijiji kwa hofu ya kuuawa na vijana
wengine wamekimbia wakiogopa kukamatwa,” alisema.
Kwa nini ipigwe ramli?
Akisimulia, Enock alisema kuna kijana
mmoja katika kijiji hicho ambaye kazi yake ni kufyatua matofali aliwaomba
vijana wanzake kuwa siku inayofuata wamsaidie kuyapanga katika tanuru.
Alisema jambo la ajabu ni kwamba
walipoamka asubuhi walikuta matofali yamekwishapangwa na haikujulikana
aliyefanya kazi hiyo.
Alisema kijana huyo na wenzake
waliamini kwamba waliofanya kazi hiyo ni wachawi.
Akisimulia kisa kingine, Enock
alisema siku chache zilizopita kuna msiba ulitokea kijijini hapo na baada ya
mazishi, siku iliyofuata walikuta msalaba umeng’olewa na haujulikani ulipo,
jambo ambalo pia lilihusishwa na ushirikina.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Ogen
Gasper aliyeomba Serikali kujenga kituo cha polisi kijijini hapo, alisema baada
ya kupata taarifa za tukio hilo alifanya jitihada kubwa kuwapata askari, lakini
hawakufika kwa kilichodaiwa ni kukosa usafiri.
Gasper alisema hilo ni tukio la tatu
kwa watu kuuawa kwa kutuhumiwa kuwa ni wachawi, la kwanza likiwa limetokea
mwaka 1996.
CREDIT: MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni