Jumanne, 7 Oktoba 2014

MASHAURI YA UKIUKWAJI WA SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA KUANZA KUSIKILIZWA ALHAMISI HII




TAARIFA

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatarajia kuendesha vikao vya Baraza la Maadili kwa ajili ya kusikiliza Mashauri yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya Viongozi wa Umma. Vikao hivyo vitaanza tarehe 9/10/2014 hadi 17/10/2014 katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Katika vikao hivyo, Baraza litapata fursa ya kusikiliza Mashauri 19 yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 katika vipengele vya matumizi mabaya ya madaraka na kutotoa Tamko la Rasilimali na Madeni.

Kimsingi, Baraza hili linafanyika baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa awali uliofanywa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa mujibu wa fungu la 
22 (2) na kujiridhisha kuwa matokeo ya uchunguzi yanaonesha kuwa kuna hoja za kutosha ambapo Viongozi wa umma husika watatakiwa kutoa maelezo mbele ya Baraza la Maadili kuhusu malalamiko yaliyotolewa dhidi yao.

Baraza la Maadili linaongozwa na Mwenyekiti Mhe. Balozi Jaji (Mst) Hamis Msumi na Wajumbe wawili Bibi Selina Wambura na Bibi Hilda Gondwe. Vikao vya Baraza hilo ni vya wazi ambapo wananchi wanaopenda kushuhudia tukio hilo wanakaribishwa.

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatoa wito kwa Viongozi wote waliopata Wito wa Kisheria unaowataka kufika mbele ya Baraza la Maadili kufanya hivyo bila kukosa kwani kukaidi Wito huo ni kinyume cha Sheria ya Maadili itakayopelekea Kiongozi huyo kukamatwa na Polisi kisha kufikishwa mbele ya Baraza 24 (4).


IMETOLEWA NA:
KAMISHNA WA MAADILI.
06 OKTOBA 2014

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni