Stanley Kolimba mbunge wa zamani jimbo la Ludewa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Manga Kata ya Madilu
Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe akiwa na Diwani wa Kata ya Madilu, Mzee Libatu akimkabidhi vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kusaidia ujenzi kwenye kata hiyo.
Na Michael Katona, Ludewa
Aliyekuwa mbunge wa Ludewa,
Stanley Kolimba amewashangaza wananchi wa kijiji cha Manga, Kata ya Madilu
wilayani Ludewa baada ya kuwaeleza kuwa anaungama dhambi zake mbele yao.
“Leo na ungama dhambi zangu
mbele ya baba Paroko hapa mbele yenu, mimi hili kanisa nalifahamu siku nyingi,
na limejengwa tangu mwaka 1968 na nilikuwa napita kwa nje, lakini kumbe kwa
ndani limeanza kuchakaa, na kwa kweli nilikuwa nahitaji nguvu kubwa, sasa leo
nimeseme kweli wabunge saba wote waliopita hapa nikiwepo na mimi, tunaposema
wengine hamna kitu nikiwepo na mimi,” alisema Kolimba.
Mbunge huyo wa zamani ambaye
hivi sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapindunzi wilayani Ludewa, alisema hayo
kufuatia ahadi aliyoitoa mbunge wa sasa wa Ludewa, Deo Filikunjombe ya
kuchangia shilingi milioni 50 kati ya shilingi milioni 75 zinazohitajika kwa
ajili ya ujenzi wa kanisa jipya la katoliki kigango cha Manga kata ya Madilu.
Kanisa hilo ambalo limejengwa
miaka ya 60 hivi sasa limepata ufa mkubwa na kuanza kuvuja kwenye paa zake,
jambo ambalo limekuwa likisababisha hofu kwa waumini huenda likaanguka.
“Mimi nimefanya kazi ya
ushirika, hapa kulikuwa na chama cha msingi, nimefanya ukaguzi miaka kenda
(tisa), ni kawa mbunge na baadaye kuwa mkuu wa wilaya, sijawahi kupata milioni
50, hivyo ni kweli kabisa kutoa ni moyo siyo utajiri, Bwana Filikunjombe kwa
kweli umenimaliza kabisa,” alisema Kolimba.
Aidha alisema yeye akiwa mbunge wa Ludewa alikuwa akipita
kwenye kata hiyo ya Madilu na kutoa msaada wa mifuko ya saruji kumi, wakati wa
ujenzi wa sekondari ya kata hiyo.
“Nilileta mifuko kumi tu ya
saruji wakati tunajenga sekondari, lazima tuseme ukweli hapa, lakini leo Filikunjombe ametoa mifuko 200 ya
saruji, ni kweli kabisa kazi anayoifanya mbunge Filikunjombe kwa sasa ni kubwa,
sisi wabunge saba tuliopita hatujaweza kuifanya,” alisema Kolimba.
Mbunge huyo aliwaambia
wananchi, “Hapa kweli hakuna mbunge mwingine yeyote aliyewahi kufanya makubwa
kama haya, nilijitahidi mimi kidogo, tena kwa kuleta mifuko mitatu mitatu ya
saruji, tunasema huyu Filikunjombe ni kiongozi wa watu. Tukubali kwamba
mwenzetu ametushinda kwa kiwango kikubwa sana.”
Wabunge waliowahi kuongoza
jimbo la Ludewa ni Violet Baraka aliyekuwa mbunge mwaka (1975 hadi 1980), John
Simalenga, Mathias Kihaule (marehemu), Holace Kolimba (Marehemu), Chrispin Mponda
(Marehemu), Stanley Kolimba, Profesa Raphael Mwalyosi na hivi sasa Deo
Filikunjombe.
Katika hatua nyingine, Mbunge
Filikunjombe akizungumza na wananchi wa kijiji cha Manga Kata ya Madilu wakati
wa kukabidhi vifaa vya ujenzi mifuko 400 ya saruji, bati 200 na vioo pamoja na
magodoro mawili, alisema ataendelea kuunga mkono jitihada za wananchi katika
kuleta maendeleo kwenye wilaya ya Ludewa.
“Serikali yetu ya CCM
inajenga shule kila kata, zahanati kila kijiji, nimekuja hapa kuwaunga mkono
jitihada zenu wananchi, ningekuta hamjafanya kitu nisingeunga mkono,” alisema
Filikunjombe.
“Nilikuja hapa nilikuta
wenzangu mnao msiba wa maendeleo, na mimi nikasema nitalia, tukaenda kushuhudia
kwa macho yangu kazi mnayoifanya, nawapongezeni sana,” aliwaambia wananchi hao.
Mbunge huyo aliwataka
wananchi hao kuwasomesha watoto wao katika maeneo ambayo amekuwa akisaidia.
“Tusomeshe watoto, mimi
nitakuwa mbunge hadi lini maisha yote, haiwezekani, itafika mahala nitasema
sasa basi, wengine waendelee, nataka mchague mbunge atakayekuja aliyesoma
sana,” alisema Filikunjombe.
Wananchi hao
walimshawishi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania mwaka 2015, lakini
Filikunjombe alisema ubunge unamtosha kwani itakuwa rahisi kuwahudumia wananchi
wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni