Jumatatu, 21 Mei 2018

AKAMATWA KWA KUJIITA YEYE NI IGP SIMON SIRRO


Maricha Mniko (30) ambaye ni mtuhumiwa aliyekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoani Njombe baada ya kufanya utapeli wa kujitambulisha yeye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro akiwa mbele ya Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Njombe, Renata Mzinga alipozungumza  na Waandishi wa Habari mjini Njombe.

JESHI la Polisi Mkoani Njombe linamshikilia mkazi wa Tandala, Wilayani Makete Maricha Mniko (30) ambaye kabila ni Mkurya na kazi yake ni dereva kwa tuhuma za kutaka kufanya utapeli kwa kujiita yeye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro na anahitaji kupata msaada wa gari ili alitumie kwa ajili ya kwenda nalo mkoani Mara.

Akizungumza kutoka ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Renata Mzinga alisema kuwa mnamo Mei 18, mwaka huu majira ya saa nne asubuhi mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Japanes ya mkoani Njombe, Daniel Hatanaka alipigiwa simu na mwananchi huyo akijitambulisha kuwa yeye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro.

"Akimweleza kuwa ana matatizo ya kijana wake ambaye anakesi huko Mara, hivyo anahitaji ampatie gari kwa ajili ya kufanya shughuli zake," alisema Renata.

Kamanda huyo alisema baada ya mmiliki huyo kupigiwa simu hiyo, aliweza kumhoji tapeli huyo kujua namba yake ameipata wapi, lakini kwa mujibu wa maelezo ya mtuhumiwa huyo alimweleza kuwa namba ya mmiliki huyo aliipata kupitia kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Njombe.

"Hivyo mmiliki huyo aliamua kuwasiliana na sisi jeshi la polisi na sisi kwa kutupa hiyo namba kwa kuwa tunazitambua hizo namba za mkuu wa jeshi la polisi, tuliona moja kwa moja kuwa siyo namba za mmiliki mkuu wa jeshi la polisi," alisema Renata.

Jumatatu, 22 Januari 2018

WANAWAKE WILAYANI MAKETE WANYIMWA HAKI YA KUMILIKI ARDHI



Na Nyandazajuublog-Makete

IMEELEZWA Wanawake wajane pamoja na wasichana wilayani Makete wamekuwa hawapewi fursa za kuweza kumiliki ardhi wilayano humo, kutokana na kuwepo na mila na desturi kandamizi zinazoendelea baina ya makabila yaliyopo.

Kufuatia hali, Katibu Tawala wa Wilaya ya Makete, Grace Mgeni amewataka wananchi wilayani Makete kuachana na tabia za kuwatenga wanawake ili wasiweze kupata haki za kuwa na ardhi, jambo ambalo alisema linaonyesha dhahiri mwanamke bado anabaguliwa.


Wilayani Makete

Akizungumza mjini hapa, mara baada ya kufungua mkutano wa wadau wa kujadili masuala ya ardhi wilayani Makete ulioandaliwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la MIICO linajishughulisha na utatuzi wa migogoro ya ardhi, Nyanda za Juu Kusini, Grace alikiri kuwa wilayani Makete bado kuna migogoro ya ardhi.

"Katika wilaya yetu ya Makete kuna changamoto ya matumizi bora ya ardhi, hasa katika upandaji wa miti, wananchi wamekuwa wanapanda miti mpaka sehemu ambazo zinatumika kwa ajili ya kilimo cha chakula, mkakati wa wilaya ni kupunguza na kutoa ile miti ambayo imepandwa sehemu zisizostahili," alisema Grace.

"...na pia kwenye umiliki wa ardhi inaonekana mwanamke hajapewa kipaumbele sana kwenye umiliki wa ardhi, jamii itambue mwanamke naye ana haki ya kumiliki ardhi kama mwanaume, tusiwatenge tuwape haki yao," alisema.

Kwa upande wake, Afisa Ardhi wa wilaya ya Makete, Novatus Lyimo alisema kutokana na sheria za kikabila kuendelea kuwepo wilayani Makete, wanawake wamekuwa hawapewi mamlaka ya kumiliki ardhi hivi sasa.

"Sheria nyingi za kimila zinabana haki mwanamke kuweza kumiliki ardhi, tunajaribu kutoa elimu kila tunapopata fursa kuwa mwanamke ana haki ya kumiliki ardhi, lakini kwa Makete bado tunachangamoto ya mwanamke kumiliki ardhi," alisema Lyimo.

"Huku bado kuna sheria za kimila, kikabilia ambazo zinawabana wakina mama, utakutana na swali mtu anakuambia mwanamke akishaolewa, ataenda kupata ardhi kwa bwana yake, lakini akifika pia kule, akifa bwana anarudi kwao, sasa hakuna sehemu ambayo anapata ardhi, hivyo hapa Makete ni changamoto," alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, hata kwenye mikutano inayoitishwa na maafisa ardhi kwa wananchi kujadili masuala ya migogoro ya ardhi, mwanamke amekuwa akinyimwa haki ya kuongea.
"Saa nyingine mwanamke kuongea kwenye mkutano hawezi kuongea, kwa sababu hizo ndizo zilivyo huku Makete, mwanaume ndiye anapaswa kuongea, kwa hiyo tunapowapa nafasi ya kuongea wanawake huwa wanashangilia sana," alisema Lyimo.

Akizungumzia namna Halmashauri inavyojikita kutatua migogoro ya ardhi wilayani Makete, Lyimo alisema bado migogoro katika halmashauri hiyo ipo licha ya kuendelea kuitatua wakishirikiana na MIICO.

"Kuna migogoro baina ya kijiji na kijiji kutokufahamu mipaka, kwa hiyo katika halmashauri yetu yenye vijiji 93 karibu  vyote vina migogoro, lakini tunaenda awamu kwa awamu, MIICO kwa upande mmoja inatusaidia sana kwa sababu kwa upande wa halmashauri kinachotubana ni bajeti," alisema Lyimo.

Naye Mratibu wa MIICO, Catherine Mulaga alisema katika utatuzi wa migogoro ya wafugaji na wakulima wamefanikiwa kusaidia kupunguza migogoro iliyokuwepo katika kata za Mbalatse na Mfumbi kwa kiasi kikubwa, lakini changamoto kubwa waliyoibaini ipo kwa upande wa wanawake kumiliki ardhi.

"Tulifanya utafiti nakuona kwamba, kulikuwa na changamoto nyingi kwenye masuala ya ardhi ambayo yana athiri, ustawi wa maisha ya mkulima wilaya ya Makete, tulikuta kuna suala la uelewa mdogo wa sheria zinazoongoza masuala ya ardhi," alisema Grace.

"Changamoto nyingine ilikuwa ni kwa upande wa umiliki wa ardhi kwa mwanamke, suala la jinsia limekuwa likijitokeza ambapo wakinamama wengi wamekuwa wakiathiriwa kwenye upatikanaji wa ardhi," alisema.

Jumatatu, 18 Desemba 2017

MKUTANO WA CCM-NEC TAIFA ULIVYOFANA DODOMA


Wajumbe wakijimwayamwaya ukumbini kushangilia wakati Mwenyekiti wa CCM Taifa, akiingia ukumbini


Mwimbaji wa TOT akiimba wimbo wa kuhamasisha mapokezi ya Mwenyekiti ukumbini


Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Jakaya Kikwete na Mwenyekiti mstaafu wa CCM Ali Hassan Mwinyi wakimsubiri Mwenyekiti Kuingia Ukumbini. Mzee Mwinyi akisoma toleo maalum la gazeti la Uhuru wakati akisubiri.


Viongozi waliotangulia meza kuu wakisimama kumlaki Mwenyekiti wa CCM rais Dk John Magufuli wakati akiingia ukumbini.


Mwenyekiti wa CCM Rais Dk John Magufuli akisalimia viongozi mbalimbali baada ya kuingia ukumbini. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein na kulia ni Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana.


Mwenyekiti wa CCM Rais Dk John Magufuli akiwa tayari ukumbini. Wengine kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Mstaafu Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu Mwenyekiti wa CCM Rais wa Zanzibar Dk. Shein, Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa CCM-bara Philip Mangula na Mwenyekiti Mstaaafu wa CCM Benjamin Mkapa.


Mwenyekiti wa CCM Rais Dk John Maguduli akijadili jambo na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Kinana baada ya kuketi ukumbini.


Waimbaji wa TOT wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya Mkutano kuanza.


Wajumbe wakiwa wamesimama kuimba wimbo wa Taifa.


Mwenyekiti wa CCM Rais Dk John Magufuli na viongozi wengine meza kuu wakiimba wimbo wa Taifa huku wamesimama. 

Jumatano, 28 Juni 2017

Viongozi wawili wa serikali wauawa Kwa Kupigwa Risasi Kibiti


Viongozi wawili wa serikali za mtaa katika Kijiji cha Mangwi wilayani Kibiti mkoani Pwani wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo Jumatano, Juni 28.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga zimeeleza kuwa waliouawa ni Mtendaji wa Kijiji cha Mangwi, Shamte Makawa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangwi, Maiko Nicholaus.

Aidha, kamanda wa polisi amesema kuwa tayari askari wamekwenda eneo hilo kwa ajili ya hatua zaidi.

Hadi sasa watu zaidi ya 37 tayari wameuawa katika mfululizo wa matukio ambayo bado Polisi hawajafahamu ni nani mhusika na lengo haswa la kufanya hivyo.