Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Samwel Sitta (Mb) aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt . Mohamed Gharib Bilal, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani, akimsikiliza Mhandisi wa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati na Madini Ephraim Mushi wakati alipotembelea banda la Wizara wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayoendelea katika viwanja vya Tangamano jijini Tanga.
Wanafunzi kutoka shule za msingi mbalimbali jijini Tanga, wakiangalia madini ya ujenzi wakati walipotembelea banda la Wizara ya Nishati na Madini katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayoendelea katika viwanja vya Tangamano jijiji Tanga.
Na Asteria Muhozya, Tanga.
Kampuni za uchimbaji madini, utafutaji mafuta na gesi wakiwemo wachimbaji wadogo nchini, wametakiwa kuzingatia sheria na kanuni za uhifadhi wa mazingira wakati wanapotekeleza shughuli zao, ili kuwezesha rasilimali zinazopatikana ardhini ziweze kuwa endelevu kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Rai hiyo imetolewa na na Mhandisi wa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Ephraim Mushi wakati wa Maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Tangamano Jijini, Tanga.
Mhandisi Mushi ameeleza kuwa, kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu duniani hususan katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ni muhimu mahitaji yao yakaenda sambamba na rasilimali zilizopo.
“Nafahamu uelewa wa makampuni ya uchimbaji madini na utafutaji wa mafuta na gesi katika usimamizi na kutunzaji wa mazingira ni mkubwa, kwani tayari kampuni hizo zina mpango wa usimamizi mazingira ambao umeeleza masuala yanayopaswa kuzingatiwa, lakini bado wanapaswa kuzingatia jambo hili wakati wote kutokana na umuhimu wa wake”, alieleza Mushi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni