TAASISI YA MISA YAWANOA WAANDISHI WA HABARI NJOMBE KUHUSU MATUMIZI YA INTANETI
Mwenyekiti wa MISA, Simon Berege akitoa mafunzo kwa mwanahabari Michael Katona kuhusu matumizi ya Intaneti yaliyofanyika Altek mjini Njombe
Mercy Sekabogo mwandishi wa habari akiwa katika mafunzo ya mtandao yaliyotolewa na MISA mjini Njombe
Na Michael Katona, Njombe
Taasisi ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika (MISA) imetoa mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari mkoani Njombe, lengo likiwa ni kuwafundisha kujua jinsi ya kutumia Intaneti.
Mafunzo hayo yanatolewa na Mwenyekiti wa Misa, Simon Berege kwa kushirikiana na Mwenyekiti Msaidizi Andrew Marawiti yakiwashirikisha waandishi wa habari wa kujitegemea pamoja na watangazaji wa redio na Luninga.
Akitoa mafunzo hayo, Berege aliwaasa waandishi hao wa habari kutoka wilaya ya Makete, Ludewa, Halmashauri ya Mji Makambako na mjini Njombe kujifunza kutumia mtandao wa Intaneti kama sehemu mojawapo ya kuweza kutafiti mambo mbalimbali katika habari wanazoziandika.
Mafunzo hayo ya MISA yanatolewa kwa lugha ya kiswahili tofauti na miaka mitatu iliyopita ambapo yalitolewa kwa lugha ya kiingereza, kusudi limekuwa ni kuwafanya waandishi wengi kuielewa vyema lugha ya kiswahili.
Vilevile mafunzo yamelenga kuwataka wanahabari hao kutumia Intaneti kwa ajili ya kufanya utafiti wa habari mbalimbali kupitia mtandao ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu vijijini.
Mbali na hilo, pia wanahabari wanatakiwa kujifunza umuhimu wa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari katika kutumia Intaneti.
Aidha wanahabari hao wanatakiwa kuzingatia usalama wa teknolojia ya habari na umuhimu wake. Kujua namna ya kutumia mitandao ya kijamii na umuhimu wake kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni