Ijumaa, 22 Mei 2015

Miaka 19 ya ajali Mv. Bukoba: Usafiri bado wa kubahatisha.

Miaka 19 ya ajali Mv. Bukoba: Usafiri bado wa kubahatisha.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Ahadi ya Rais kikwete haijatekelezwa.
Sehemu ya chini ya meli ya MV Bukoba iliyozama katika Ziwa Victoria na kuua mamia ya watu.
Ni kawaida kwa nchi yeyote kama ilivyo kwa watu binafsi, kuwa na utaratibu wa kuadhimisha matukio yaliyo muhimu katika historia ama maisha ya nchi zao, watu binafsi, jumuiya au  taasisi.
 
Kwa ujumla, sherehe ama maadhimisho ya matukio ya aina hiyo muhimu, huweza kufanyika kwa namna mbili.
Kufanya kumbukumbu ya tukio au matukio ya furaha kwa upande mmoja, ama kumbukumbu ya tukio au matukio ya huzuni kwa upande mwingine.
 
Ni kwa misingi hiyo, leo ni kumbukumbu ya miaka 19, tangu itokee ajali ya kuzama kwa meli ya Mv. Bukoba.
Meli hiyo, ilizama tarehe kama ya leo, yaani Mei 21 mwaka 1996, na kuua watu zaidi ya 700, wakati ilipokuwa ikitokea Bukoba, kwenda Mwanza.
 
Ajali hiyo ilitokea alfajiri, umbali wa karibu kilometa 30, kutoka bandari ya jijini Mwanza.
Meli ya Mv. Bukoba iliundwa na kampuni ya Kibelgiji, na ikazinduliwa Julai 27, mwaka 1979, kwa maana hiyo ilizama ikiwa na umri wa miaka 17 tu, toka kutengenezwa kwake. 
 
Inasemekana kuwa, ilibainika haikuwa thabiti na ilikosa uwiano tokea siku ilipozinduliwa.
Ilikuwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 850, na abiria 430.
 
Kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Jaji Robert Kisanga, iliyoundwa kuchunguza chanzo cha ajali ya meli hiyo, ilikuwa imepakia abiria kati ya 750 na 800 pamoja na wafanyakazi 37 siku ya ajali.
 
Kati ya hao, 114 waliokolewa wakiwa hai, wakati 391 waliopolewa wakiwa wamefariki na kuzikwa katika makaburi ya Igoma, nje kidogo ya Jiji la Mwanza.
 
Aidha, miili mingine ilichukuliwa na jamaa zao kwa ajili ya mazishi katika maeneo walikotoka.Hata hivyo, jumla ya miili 332 haikupatikana.
 
 Kimsingi chanzo cha ajali hiyo kinasemekana kuwa ni hitilafu katika injini ya meli hiyo, sababu haikufanyiwa ukaguzi.
Serikali ilichukua hatua za kumshitaki aliyekuwa nahodha wa Mv. Bukoba, Jumanne Mwiru, ambaye kwa sasa ni marehemu, na Mkaguzi wa Mamlaka ya Bandari, Gilbert Mokiwa.
 
Aidha iliwashitaki pia aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Bukoba, Alphonce Sambo, na aliyekuwa Maneja wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila.
 
Shauri hilo Namba 22, la mwaka 1998, lilianza kusikilizwa Mei 14, mwaka 2001, na miongoni mwa waendesha mashitaka katika shauri hilo, alikuwa ni Eliezer Feleshi, aliyekuja kuwa mwendesha mashtaka mkuu wa serikali, kabla ya kuwa jaji wa mahakama kuu, nafasi ambayo anaishikilia hadi sasa.
 
Hukumu ya kesi ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Juxton Mlay (sasa mstaafu), Novemba 29, mwaka 2002.
 
Washitakiwa wote walishinda kesi, kufuatia hukumu ya kurasa 118, iliyosomwa kwa dakika 160 na Jaji huyo.
 
Katika hukumu yake hiyo, jaji Mlay alisema meli ya Mv. Bukoba, ilizama kwa sababu haikuwa na uwiano wa majini, na siyo uzembe wa washitakiwa.
 
HALI ILIVYO SASA
Hadi tunapokumbuka tukio hilo leo hii, bado usafiri wa maji katika ziwa Victoria, umebaki kuwa na changamoto kubwa, kutokana na ukweli kuwa hakuna meli ya uhakika inayotoa huduma katika ziwa hilo kwa sasa.
 
Na hasa ikichukuliwa kwamba, usafiri wa maji katika ziwa hilo, ni mkombozi kwa watu wengi wa kanda ya ziwa, hasa wanaoishi katika visiwa, ndani ya ziwa hilo.
 
 Pia pamoja na wananchi wanaofanya safari zao kati ya Bukoba na jiji la Mwanza, wananchi ambao kipato chao ni kidogo, wakulima na wafanyabiashara katika ukanda huo wa ziwa. 
 
Kama ilivyoonyeshwa hapo juu, meli hiyo ilikuwa na uwezo wa kubeba tani 850 za mizigo na hivyo ilikuwa ni tegemeo kubwa kwa wakulima na wafanyabiashara katika kanda hiyo.
 
Na ndiyo maana baada ya kuzama kwake, tegemeo pekee lililokuwa limebakia ni kwenye meli ya Mv. Victoria, ambayo nayo ni ‘supana mkononi.’
 
Ni ‘supana mkononi’ kwa kuwa, mwezi Oktoba mwaka jana, abiria 381 waliokuwa katika meli hiyo, nao walinusurika kufa, baada ya chombo hicho kilichokuwa kikifanya safari kutoka Bukoba kwenda jijini Mwanza, kuzimika ghafla.
 
Meli hiyo ilipata hitilafu katika usukani, na baadaye injini zake kuzimika zaidi ya mara mbili, kabla ya kujikongoja hadi bandari iliyo karibu ya Kemondo.
 
Uchakavu wa Mv. Victoria umelalamikiwa kwa muda mrefu, lakini hakuna juhudi za maana zilizochukuliwa kuhakikisha kuwa meli hiyo inafanyiwa matengenezo ya kueleweka.
 
TEGEMEO KWA RAIS KIKWETE
Sasa wananchi wa kanda hiyo na hasa wanaotumia usafiri wa maji ndani ya ziwa Victoria, wakiwamo ndugu na jamaa ya waliopoteza wapendwa wao ambao leo, tunawakumbuka, waliweka tegemeo kubwa kwa Rais Dk. Kikwete kuwa, atawatatulia tatizo hili.
 
Na ikumbukwe kuwa yeye mwenyewe alitoa ahadi ya kuwaondolea kero hiyo, wakati wa kampeni zake za urais mwaka 2010.
 
Katika kampeni hizo, Dk. Kikwete aliahidi kununua meli kubwa kuliko ile ya Mv. Bukoba, iliyozama mwaka huo wa 1996.
Aliahidi kufanya hivyo akisema kwamba, anaelewa ubovu wa meli ya Mv. Victoria, pamoja na meli zingine zinazotoa huduma ya usafiri wa maji ndani ya ziwa hilo.
 
Sasa Dk. Kikwete yu mbioni kumaliza ngwe yake mwaka huu, na siku ndiyo zinazidi kuyoyoma, huku ahadi ya meli aliyoahidi kuwapatia wakazi wa kanda hiyo tangu mwaka 2010, ikiwa bado haijatekelezwa.
 
Tunasema Dk. Kikwete kwa sababu, ndiye aliyetarajiwa na wananchi wa kanda ya ziwa kuwaletea meli mpya ya kuwakomboa kutokana na adha ya vifo, na upotevu wa mali utokanao na dhoruba za ziwa hilo.
 
Dhoruba kama za hali ya kupotea njia, upepo mkali, na vyombo kupinduka.
 
Kwamba kutokana na kukosekana kwa meli ya uhakika katika ziwa hilo, kumewafanya wananchi wategemee usafiri wa mitumbwi usio wa uhakika.
 
Hauna uhakika kwani, hali ya hewa inapobadilika na ziwa kuchafuka, basi wasafiri hulazimika kupunguza mizigo kwa kuitosa ziwani, na kwamba pale mambo yanapokuwa mabaya zaidi, hubidi watu kutosana wenyewe kwa wenyewe hadi mtumbwi utulie.
 
Ni ukweli ulio dhahiri kwamba, Dk. Kikwete ametoa ahadi nyingi kwa wananchi wake katika maeneo mbalimbali ya nchi aliyoyatembelea, kama sehemu ya kujinadi ili wananchi wampe ridhaa ya kuwaongoza.
 
Na ni kweli vilevile kwamba, ametekeleza ahadi nyingi kati ya zile alizoziahidi.
 
Lakini ni ukweli vile vile kuwa, kuna ahadi nyingi ambazo bado hajazitekeleza hadi sasa, wakati anapoelekea kukabidhi kijiti kwa mtanzania mwingine wa kuliongoza taifa hili.
 
Ni rai basi ya andiko hili kwa Rais Dk. Kikwete, akatimiza ahadi yake ya kuwapatia wakazi wa kanda ya ziwa, na hasa wanaotumia usafiri wa maji ndani ya ziwa Viktoria, meli aliyoiahidi wakati tunapokumbuka tukio hilo kubwa la ajali ya Mv. Bukoba leo.
 
Yako mengi ya kumkumbuka Dk. Kikwete aliyoyafanya katika eneo hilo la nchi, hasa upande wa miundo mbinu, kama barabara, lakini kuwapatia meli wakazi wa eneo hilo, kabla ya kuondoka madarakani, itakuwa ni kumbukumbu na alama kubwa ya namna alivyoweza kutimiza ahadi yake.
 
Pamoja na kuwa imebaki miezi mitano ya utawala wake, kipindi hicho kinatosha kutimiza ahadi hiyo, ambayo itakuwa faraja kubwa, si kwa waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo tu, bali wananchi wote wa ukanda huo.
SOURCE: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni