Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Saidi Meck Sadiki akizungumza na watendaji , waganga wakuu wa wilaya na mkoa wa mkoa wa Dar es salaam leo wakati akizindua Mpango Kazi wa kuharakisha kupunguza vifo vya akina mama na watoto walio chini ya miaka 5 kwa mkoa wa Dar es salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema akizungumza na watendaji , waganga wakuu wa wilaya na mkoa wa Dar es salaam leo kueleza nafasi yake katika kusimamia utekelezaji wa wakati Mpango Kazi wa kuharakisha kupunguza vifo vya akina mama na watoto walio chini ya miaka 5 kwa mkoa wa Dar es salaam.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Grace Maghembe akiwasilisha mpango Kazi wa Kuharakisha kupunguza vifo vya akina mama, Watoto wachanga na watoto walio chini ya umri wa miaka 5 kwa mkoa wa Dar es salaam.
Baadhi ya watendaji wa mkoa , waganga wakuu wa wilaya na mkoa wa Dar es salaam waliohudhuria uzinduzi wa Mpango kazi wa Kupunguza Vifo vya akina mama wajawazito na Watoto chini ya miaka 5 leo wakimsikiliza Mkuu wa mkoa huo Mhe. Sadiki Meck Sadiki (hayupo pichani) Picha/Aron Msigwa.
RC DAR ES SALAAM AZINDUA MPANGO KAZI WA KUHARAKISHA KUPUNGUZA VIFO VYA AKINA MAMA NA WATOTO CHINI YA MIAKA 5 AKEMEA WATUMISHI WAZEMBE.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Saidi Meck Sadiki amezindua Mpango Kazi wa kuharakisha kupunguza vifo vya akina mama na watoto walio chini ya miaka 5 kwa mkoa wa Dar es salaam na kukemea tabia ya baadhi ya watumishi wasio waadilifu wanaotumia lugha za kuudhi, kejeli na vitendo vya unyanyasaji kwa akina mama wajawazito wanaofika kupata huduma za uzazi katika hospitali, vituo vya afya na Zahanati.
Akizungumza katika kikao kilichowahusisha watendaji wa mkoa , waganga wakuu wa wilaya na mkoa wa Dar es salaam leo jijini Dar es salaam, Mhe. Sadiki amesema watumishi wa afya wa mkoa huo wanao wajibu wa kutekeleza majukumu yao na kutimiza malengo yaliyowekwa na Serikali ya kuwapatia huduma bora za afya akina mama wajawazito na watoto walio na umri chini ya miaka 5 yaliyowekwa na mkoa.
Amesema kuwa katika kutekeleza mpango kazi huo Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria watumishi wa afya watakaobainika kushiriki katika vitendo ubadhirifu na wale watakaosababisha kwa namna moja au nyingine vifo vya mama wajawazito na watoto chini ya miaka 5 watakaofika hospitalini kupata huduma za afya na kupoteza maisha yao kutokana na uzembe wa watumishi katika vituo husika.
Amebainisha kuwa mkoa Dar es salaam pamoja na mambo mengine umeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa inawafikia akina mama na watoto na kuwapatia huduma bora akina mama wajawazito wanaofika katika vituo vya afya vya Serikali kupata huduma za uzazi ili kukabiliana na vifo vya akina mama na watoto vinavyotokea.
Ameeleza kuwa Tanzania imekuwa ikitekeleza malengo ya millennia (MDG)ambayo yalipangwa kukamilika ifikapo Desemba 2015 na kuongeza kuwa katika utekelezaji wa malengo hayo bado inakabiliwa na changamoto za kupunguza vifo vya wajawazito ambavyo amesema kwa takwimu za mwaka 2013 zinaonyesha vifo 410 kwa kila vizazi hai 100,000.
“ Tanzania katika jambo hili tumepiga hatua japo bado tunakabiliwa na changamoto ya kuendelea kupunguza vifo hivyo kufikia 133 kwa kila vizazi hai 100 if ikapo mwezi Desemba 2015”
Amesema akiwa kiongozi wa mkoa huo atahakikisha lengo hilo linatimiza kabla ya muda uliopangwa na kuwataka watendaji wa afya kwa ngazi zote kutimiza wajibu wao ipasavyo na kuzitumia rasilimali zilizopangwa kutekeleza malengo yaliyopangwa ili kuhakikisha kuwa vifo vinavyotokana na uzazi na vile vya watoto wachanga vinapungua .
“Nachoweza kusema, uwezo wa kukabiliana na changamoto hii tunao tukiunganisha nguvu zetu kwa mazingira tuliyonayo ya taasisi za Serikali na Binafsi bado tunayo nafasi nzuri ya kutimiza malengo yaliyowekwa, kwa sasa tunaendelea na mkakati wetu wa kuongeza wodi za kujifungulia akina mama wajazito wilaya ya Temeke, Ilala na Kinondoni ili kuongeza wigo wa huduma za afya” Amesemaa.
Ametoa wito kwa wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa akina mama wajawazito ili waweze kuelewa umuhimu wa kuhudhuria Kliniki kabla na baada ya kujifungua za afya kupitia mpango wa TIKA utakaoanzishwa katika jiji la Dar es salaam utakaowawezesha kupata huduma za afya kwa mwaka mzima kwa gharama nafuu.
Katika hatua nyingine Mhe. Sadiki amewataka wakurugenzi wa manispaa za Dar es salaam kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya motisha kwa watumishi wa afya wanaotumia muda mwingi kazini wakiwahudumia wagonjwa hususani akina mama wachanga na watoto chini ya miaka 5 wa mkoa huo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Grace Maghembe awali akiwasilisha Mpango Kaziwa Kuharakisha kupunguza vifo vya akina mama, Watoto wachanga na watoto walio chini ya umri wa miaka 5 kwa mkoa wa Dar es salaam amesema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali toka kuzinduliwa kwake miaka 2 iliyopita na Rais Jakaya Kikwete umepata mafanikio.
Amesema kuwa pamoja na kuongezeka wa idadi ya wazazi wanaojifungua kutoka 97,807 hadi 134,838 mwaka 2012 hadi 2014 vifo vya uzazi vimepungua kutoka 123 hadi 99 katika vizazi hai 100,000.
Amesema mafanikio zaidi ya huduma ya afya ya mama na mtoto katika mkoa wa Dar es salaam bado yanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kiwango kidogo cha matumizi ya huduma ya uzazi wa mpango wa asilimia 47, kiwango kidogo cha asilimia 51 ya wajawazito wanaohudhuria Kliniki angalau mara 4 chini ya lengo kitaifa ambalo ni asilimia 90.
Aidha ameeleza kuwa mkoa unaendelea kuchukua hatu mbalimbali za kuhakikisha kuwa huduma ya afya ya mama na mtoto inaimarika katika jiji la Dar es salaam kwa kuiweka huduma hii kuwa kipaumbele cha mkoa na kuongeza usimamizi shirikishi wa huduma za afya, mafunzo kazini kwa watumishi, kuongeza vitendea kazi, dawa na vifaa tiba pamoja na kuhamasisha ushiriki wa wadau na wafadhili mbalimbali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni