Marehemu Chigwele Che Mundugwao amewahi kulipatia taifa sifa kimataifa katika nchi za Scandinavia ambako alijipatia mialiko mbalimbali ya kuwaburudisha mashabiki wake wa muziki.
Miongoni mwa bendi ambazo amewahi kuimbia ni pamoja na Tatu Nane.
Marehemu Che Mundugwao aliyezaliwa mwaka 1968 amefariki akiwa na umri wa miaka 47.
UNDANI WA CHE MUNDUGWAO
Chingwale Che Mundugwao (47) hadi anapatwa na umauti alikuwa mahabusu akikabiliwa na kesi ya wizi wa hati za kusafiria 26 (Passports) mali ya serikali tangu aliposhitakiwa rasmi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Juni 2, 2013, akiwa na wenzake 8.Washitakiwa wengine ni wahudumu wa Idara ya Uhamiaji Adam Athuman na Abdallah Salehe. Raia wa Uingereza Ahsan Iqbal au Ali Patel, Ofisa Ugavi wa Idara ya Uhamiaji Shemweta Kiluwasha, Injinia Keneth Pius wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, mfanyabiashara Ally Jabir, Rajab Momba na Haji Mshamu.
Makosa waliyokuwa wakishitakiwa nayo yalikuwa na dhamana lakini Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwendendo wa Makosa ya Jinai ya Mwaka 2002 , aliwanyima dhamana hivyo kusota gerezani kwa kipindi chote hicho hadi Che alipougua maradhi ya damu na kupelekwa hospitali ya Taifa ambako alipatwa na mauti baada ya kulazwa kwa muda mrefu. Che Mundugwao alikuwa mahabusu wa Gereza la Keko jijini Dar es salaam .
Aidha, wakati akiwa gerezani, Che Mundugwao alifiwa na mtoto wake lakini hakuweza kushiriki msiba wake kwasababu alikuwa gerezani chini ya ulinzi na leo masikini amemfuata mwanae mavumbini!.
Binafsi Che Mundugwao nilianza kumfahamu tangu Kipindi kile akiwa mwanamuziki wa muziki wa asili na aliwahi kupiga wimbo wake mmoja uliompatia umaarufu unaitwa 'TUMETOKA KWETU MAHENGE....TUMEKUJA DAR ES SALAM KUJA KUCHEZA SINDIMBA '. Mwaka 2000.
Wimbo huu ulitamba katika miaka ya 1990 na wanamuziki waliocheza ni pamoja na Luiza Mbutu ambaye kwa sasa ni kiongozi wa Bendi ya African Stars “Twanga Pepeta”. Kwa mtakaoenda kutaza video ya wimbo huo mtakubaliana nami kuwa Luiza Mbutu ametoka mbali katika fani ya muziki na amebadilika sana.
Aidha Che Mundugwao aliendesha Kipindi cha Muziki wa Asili Katika Redio Tumaini na hatimaye mwisho wa siku Juni 3 mwaka 2013, Mimi nilipokuwa Mwandishi wa Habari za Mahakamani wa Gazeti la Tanzania Daima, nilishuhudia Che Mundugwao akipandishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza mchana, akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu na kupandishwa kizimbani na kushitakiwa kwa kesi hiyo.
Nilisikitika sana kuona Che Mundugwao yuko mikononi mwa dola na nilikuwa sina jinsi ya kumsaidia kwa sababu licha ya kuwa ni rafiki yangu sikua na cha kumsaidia, Sheria ni Msumeno!
Mungu aiweke roho ya marehemu mahali panapostahili. Amina.
Ndugu msomaji, Marehemu Che Mundugwao mbali ya kuwa na kipaji cha sanaa na utangazaji hapa nchini, mimi binafsi nitamkumbuka kwa ucheshi wake na hata kwa ushauri mkubwa aliokuwa akiutoa. Mungu akupumzishe kwa amani Che Mundugwao
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni