Jumatatu, 23 Machi 2015

UDA SASA TAABANI KIFEDHA

SHARE THIS
TAGS
UDANa Mwandishi wetu, Dar es Salaam
WAKATI Serikali ikitafakari kulipatia Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) haki ya kuendesha mradi mkubwa wa mabasi yaendayo kasi katika Jiji la Dar es Salaam, kuna habari kuwa shirika hilo linaelekea kufilisika.
Habari za uhakika kutoka ndani ya shirika hilo zimebainisha kuwa kwa sasa UDA liko katika hali mbaya kifedha kiasi cha kushindwa kumudu gharama za kujiendesha, ikiwamo kushindwa kuwalipa wafanyakazi wake mishahara.
Chanzo hicho cha habari kililiambia MTANZANIA kuwa wafanyakazi wa UDA hawajalipwa mishahara yao tangu mwaka huu uanze na hali yao ya maisha ni ngumu na ya kusikitisha mno.
Uchunguzi zaidi wa gazeti hili umebaini kuwa kutetereka kifedha kwa UDA linalomilikiwa kwa sehemu kubwa na kampuni ya Simon Group chini ya Mwenyekiti Mtendaji Robert Kisena, kumechangiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na baadhji ya wabunge kudaiwa kuligeuza shirika hilo kama mradi wao wa kuchota mamilioni ya shilingi.
Taarifa zaidi zimedai kuwa kuna magari 50 katika yadi ya UDA iliyopo Kurasini Dar es Salaam ambayo yamekosa fedha za kulipia vibali vya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), bima na Mamlaka ya Udhibiti wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kwa sababu ya ukata.
Pia magari mawili yaliyoingizwa nchini na shirika hilo kwa ajili ya mradi wa majaribio wa mabasi yaendayo kasi (DART)yamekwama bandarini kwa sababu ya ukosefu wa fedha za kuyalipia.
“Mwandishi mambo yanayofanyika hapa ni ya ajabu sana, viongozi wa serikali wakiwamo mawaziri, wabunge, viongozi wa polisi na viongozi wa CCM wanapishana kila siku kuja kuchota mamilioni kutoka UDA kana kwamba ni mashine ya ATM, yaani wameligeuza shirika hili kama taasisi ya misaada na siyo biashara.
“Mambo yale yale yaliyosababisha kufa kwa mashirika na kampuni za umma zilizoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ndiyo yanayoliyumbisha kifedha leo shirika letu la UDA,” kinabainisha chanzo chetu cha habari na kuongeza:
“Mwenyekiti wetu anamwaga fedha kwa viongozi wa Serikali na CCM ili kupata ulinzi kutoka kwao kwa sababu anahofia kunyang’anywa kutokana na kudaiwa kuwa alilinunua shirika kwa njia zisizo halali ikiwamo utoaji rushwa.”
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa nusu ya mabasi ya shirika hilo hayatembei kutokana na kukosa fedha za kununulia vipuri na upungufu wa mafundi kwa sababu inadaiwa kuwa nusu ya idadi ya mafundi wa UDA hawahudhurii kazini na waliopo hawafanyi kazi wakitaka kulipwa mishahara yao.
Msemaji Mkuu wa UDA, George Maziku, alikanusha madai akisema hakuna mfanyakazi ambaye hajalipwa mishahara ya miezi mitatu.
Alisema wafanyakazi wote wanadai mshahara wa Februari tu ambao alisema umechelewa kutokana na kuwapo marekebisho ya mfumo wa uhasibu katika shirika hilo.
“Siyo kweli kwamba UDA ipo hoi kifedha au inaelekea kufilisika, tupo imara kiuchumi na shughuli zetu zinasonga mbele kama kawaida. Kuhusu wafanyakazi kutolipwa mishahara tangu Januari.
“…hili nalo halina ukweli wowote, wafanyakazi hatujalipwa mshahara wa Februari pekee ambao umechelewa kidogo kutokana na marekebisho kadhaa ya mfumo wa uhasibu,” alisema Maziku.
MTANZANIA ilipomtafuta Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group, ambao ndiyo waendeshaji wa UDA, Robert Kisena, alisema halitambui suala hilo na hakuna viongozi wa Serikali wala wabunge wanaofika ofisi kwake kuchukua fedha.
“Nichokwambia hakuna kitu kama hicho. Jiji la Dar es Salaam limekuwa na maneno kuna watu kazi yao ni kutunga uongo hilo si kweli.
“Suala la mishahara waulizwe idara ya uhasibu na hilo la magari kukwama bandari… yapo kwenye utaratibu wa kutolewa,” alisema Kisena.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni