Jumatano, 18 Machi 2015

MAKALA YA SHERIA: ILI KUBADILI HATI YA NYUMBA / KIWANJA KWA HARAKA ANDAA NYARAKA HIZI


Watu wengi wanaonunua ardhi wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa katika kubadili majina yaani kutoka mmiliki wa mwanzo kwenda kwa mmilki mpya aliyenunua. Upo usumbufu ambao husababishwa kwa makusudi na maafisa wanaohusika lakini pia upo usumbufu ambao husababishwa na watu wenyewe wanaotaka kubadili majina. Awali ya yote lazima nikiri kuwa baadhi ya maafisa wa mamlaka za ardhi husababisha uchelewaji kwa makusudi kabisa na lengo likiwa kujenga mazingira ya kupozwa kidogo. Hili lipo na kila mtu ambaye amekuwa akishughulikia masuala ya hati na kubadili majina miliki kama mimi atakiri kukutana na haya. Hao tuwaache mimi leo nazungumzia maandalizi ambayo ukiyafanya mapema utafanikiwa kwa urahisi na haraka kubadili jina la kiwanja au nyumba kutoka kwa mtu akiyekuuzia kuingia jina lako.

1.UMUHIMU WA KUBADILI JINA HARAKA BAADA YA MANUNUZI.

Sheria iko wazi kuwa ambaye jina lake linaonekana kwenye hati ndiye mmiliki.

Kwa kauli hii mnunuzi anatakiwa kufanya jitihada za haraka na za makusudi kubadili jina mara tu baada ya kununua kiwanja au nyumba. Sikatai kuwa kunakuwa na mkataba wa mauziano lakini lazima ieleweke kuwa mbele ya macho ya sheria jina lililo kwenye hati lina uzito kuliko mkataba wa mauziano. Usiridhike kukaa na mkataba wa mauziano ikiwa hujabadili jina. Hii ni kwa ajili ya ulinzi wako na wa ardhi yako. Utakapotokea mgogoro wa umiliki ikiwa hujabadili jina waweza kuwa katika hatari kubwa ya kupoteza hasa kama mgogoro huo umeanzishwa na aliyekuuzia. Huu ndio ukweli na lazima tuonyane ili tuwe salama na mali zetu. Lakini pia hata ukitokea mgogoro mwingine wowote wa umiliki kuna mambo ndani ya sheria yataufanya kuwa mgumu kutokana na sababu tu kuwa ulikuwa hujabadili jina. Hapo sijaongelea faida nyingine za kubadili jina kama kukopa n.k. Nishauri tu kwa ufupi kuwa unapojiandaa kununua nyumba au kiwanja jiandae pia na kubadili jina moja kwa moja. Hakikisha haya mawili yanakwenda pamoja.

2. ILI KUBADILI HATI KWA URAHISI NA HARAKA HEBU ANDAA NYARAKA HIZI.

( a ) NYARAKA ZA UHAMISHO
Nayaraka za uhamisho zinajumuisha fomu namba 29 ijulikanayo kama fomu ya kusudio la uhamisho( notification of disposition) ambayo hueleza nia na lengo la muuzaji kutaka kubadili jina au kuondoa jina lake katika hati. Hii utaandaa nakala tatu . Pili ni fomu namba 30 ambayo hujulikana kama fomu ya idhibati ya uhamisho ( application for approval of disposition). Katika fomu hii muuzaji pia atakuwa anatoa idhini kwa mamlaka za ardhi kuidhinisha hiari yake ya kuachia umiliki kutoka kwake kwenda kwa mtu mwingine ambaye ndiye mnunuzi. Mwisho ni fomu namba 35 ijulikanayo kama fomu rasmi ya kuhamisha umiliki ( transfer of a right of occupancy) ambayo ndiyo rasmi sasa huhamisha umiliki kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuzi. Hii ndiyo humpa mnunuzi umiliki rasmi . Pia mkataba wa mauziano ni nyaraka ambayo itaambatanishwa hapa.

Kwa kiwanja au eneo ambalo halijaendelezwa ( halijajengwa) huandaliwa kitu kiitwacho commitment bond kikiwa kama ziada ya nilivyotaja hapo. Fomu zote hizo pamoja commitment bond hupatikana katika ofisi za wanasheria na huandaliwa na wanasheria.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni