Jumatano, 21 Januari 2015

CHUO CHA ELIMU YA BIASHARA (CBE) CHATOA MSAADA WA MASHUKA HOSPITALI YA WAZAZI META.

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE) Profesa Emmanuel Mjema(kushoto) akimkabidhi moja ya mashuka Mkuu wa Idara ya Hospitali ya Wazazi Meta, Dk. John France walipotembelea hospitali hiyo.


Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE) Profesa Emmanuel Mjema(kushoto) akimuonesha  shuka Mkuu wa Idara ya Hospitali ya Wazazi Meta, Dk. John France walipotembelea hospitali hiyo na kutoa msaada wa Mashuka.

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE) Profesa Emmanuel Mjema akisaidiana na baadhi ya Watumishi wa Hospitali ya Wazazi Meya kutandika kitanda kwa kutumia Shuka lililotolewa na Chuo cha Elimu ya Biashara katika kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Mkuu wa Idara ya Hospitali ya Wazazi Meta, Dk. John France ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, akishukuru kwa msaada uliotolewa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE)

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE) Profesa Emmanuel Mjema(kushoto) akimfariji mgonjwa Martha Mwakajila walipotembelea hospitali hiyo na kutoa msaada wa Mashuka.

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE) Profesa Emmanuel Mjema, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kutoa msaada wa mashuka katika Hospitali ya wazazi Meta.

Muonekano wa mashuka yaliyotolewa na Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE) likiwa limetandikwa kitandani.

Baadhi ya wagonjwa wakiwa wamelala katika Wodi namba 4 ambalo limenufaika na Msaada wa Mashuka kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE).



CHUO cha Elimu ya Biashara(CBE) kimetoa msaada wa mashuka katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kitengo cha Wazi Meta ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE), Profesa Emmanuel Mjema, alisema msaada huo unagharimu shilingi Milioni tano ikiwa ni sehemu ya kushiriki huduma za kijamii katika maadhimisho ya miaka 50.

Alisema Chuo hicho kilianzishwa Januari 21, 1965 hivyo hadi sasa kinakuwa kikitimiza miaka 50 ambapo Chuo kinaadhimisha mafanikio hayo kwa kushiriki huduma za jamii kama mchango wake katika jamii ambapo mbali na kutoa msaada wa mashuka katika hospitali ya Wazazi Meta pia walitembelea Hospitali ya Mkuranga.

Alizitaja shughuli zingine kuwa ni kutoa elimu ya ujasiliamali kwa vijana wa Mkoa wa Dar es salaam na Dodoma, elimu kwa wanaojiandaa kustaafu ili wawe na maandalizi ya kukabiliana na maisha baada ya kustaafu.

Mbali na msaada huo, Profesa  Mjema alitoa wito kwa wafanyabiashara nchini kujenga utamaduni wa kuhudhuria masomo ya ujasiliamali ili waweze kufanya biashara zenye uhakika kwa kuweza kukokotoa faida na hasara tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wao hufanya biashara kwa mazoea.

Alisema Vyuo vya CBE vinatoa nafasi za masomo ya jioni ambayo yatamwezesha mfanyabiashara yeyote kuweza kujiendeleza kielimu hivyo kuweza kuimarisha biashara yake baada ya kupata elimu itakayomfanya aendeshe biashara kifaida.

Naye Mkuu wa Idara ya Hospitali ya Wazazi Meta, Dk. John France, ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, aliupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kuiona Hospitali ya Wazazi Meta na kutoa msaada wa mashuka.

Alisema msaada huo utasaidia kuboresha mazingira ya Hospitali pamoja na kuongeza ari ya utendaji kazi kwa watumishi kutokana na kufarijiwa na taasisi mbali mbali na kutoa misaada yao kutokana na kuwepo kwa hospitali nyingi zenye mahitaji tofauti lakini uongozi wa benki ukaiona Hospitali ya Wazazi ya Meta.

Aliongeza kuwa Chuo cha CBE kinatoa changamoto kwa taasisi zingine za umma kuona umuhimu wa kutembelea wagonjwa na kutoa msaada kwani jambo hilo limezoeleka kufanywa na taasisi za watu binafsi na mashirika ya dini hivyo kuzikumbusha taasisi za Serikali pia kujenga utamaduni wa kutoa misaada kwa wahitaji.

Alisema katika matibabu ya wagonjwa mbali na kutoa dawa lakini Mgonjwa hupona baadhi ya matatizo kutokana na kutembelewa na kufarijiwa ambapo alitoa wito kwa watu na taasisi zingine kuwa na utamaduni wa kuwatembelea wagonjwa na kuwafariji.

Wakati huo huo, fomu za kujiunga na Chuo hicho katika ngazi za Cheti na Diploma kwa mwaka wa masomo 2015 zimeanza kutolewa Chuoni hapo Forest ya zamani katika majengo ya Chuo Kikuu Huria jijini Mbeya.

Aidha masomo yanatarajia kuanza mwezi Machi Mwaka huu, Watu wote mnakaribishwa katika Chuo cha Elimu ya Biashara Kampasi ya Mbeya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni