Jumatatu, 6 Oktoba 2014

MKURUGENZI TFF AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA SITA JELA, ANUSURIKA BAADA YA KULIPA FAINI YA MILIONI 3/=!

 
 Wakili Eric Nyato (mwenye mkoba) kutoka kampuni ya Uwakili ya Mushokorwa, akitoka mahakamani kwenda kujadiliana na mteja wake Eliud Peter Mvela Wamahanji (kushoto) mara baada ya huku
 
Na Daniel Mbega, Iringa
MKURUGENZI Msaidizi wa Sheria na Uanachama wa Shirikisho la Kandanda nchini (TFF), Eliud Peter Mvela Wamahanji, amehukumia kifungo cha miaka sita jela au kulipa faini ya Shs. 3 milioni baada ya kupatikana na hatia kutenda makosa manne.
Hata hivyo, Wamahanji amenusurika kutumikia kifungo hicho cha miaka sita jela
baada ya kulipa faini kwa fedha taslim mahakamani hapo kupitia kwa wakili wake Erick Nyato wa kampuni ya uwakili ya Mushokorwa na kupewa stakabadhi yenye nambari 3425607, huku ‘Defender’ la Polisi likiwa linamsubiri tayari kumpeleleka gerezani ikiwa angeshindwa kulipa.


Akitoa huku hiyo leo alasiri, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Iringa, Ruth Massam, amesema mshtakiwa amekutwa na hatia katika makosa manne ambapo mahakama imejiridhisha pasipo shaka na hivyo kutoa adhabu hiyo ili liwe fundisho kwa wengine wanaokwenda kinyume na sheria za nchi.
 
Kwa mujibu wa sheria, mshtakiwa kama angeshindwa kulipa faini hiyo, angekaa jela kwa kipindi cha miaka miwili, kwani hukumu zote zinatumikiwa kwa pamoja.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo, Hakimu Massam alisema, upande wa utetezi umeshindwa kutoa ushahidi wa kuridhisha kwa makosa manne aliyoshtakiwa nayo ambapo kosa la kwanza ni kuendesha biashara ya bima bila kibali; kosa la pili ni kufanya shughuli za bima bila usajili; kosa la tatu ni kuuza stika za magari za bima na Cover Note bila kibali’ na kosa la nne ni kutoa stakabadhi za bima bila kibali.
 
Mshtakiwa alidaiwa kutenda makosa hayo mnamo tarehe 25 Mei, 2013 katika Jengo la Highland Hall katika Manispaa ya Iringa huku akitumia kampuni ‘hewa’ ya IMOCK.
“Adhabu kwa kosa la kwanza ni faini ya Shs. 1 milioni au kifungo cha miaka miwili gerezani na kosa la pili adhabu yake ni Shs. 1 milioni au kifungo cha miaka miwili jela.
“Adhabu kwa kosa la tatu na la nne ni kifungo cha mwaka mmoja au faini ya Shs. 500,000 kwa kila moja,” alisema Hakimu Massam.
 
Awali, Hakimu Massam alisema mshtakiwa alitenda makosa hayo kwa kutumia kampuni ya Bima ya Mwananchi yenye makao yake makuu Arusha bila ya kuwa mwajiriwa wa kampuni hiyo.
 
 “Mshtakiwa alikutwa na vifaa hivyo kwenye ofisi iliyopo Jengo la Highland ikiwa haina kibao cha jina la kampuni lakini kwenye stakabadhi ikionyesha kuwa inafanya kazi za Kampuni ya Mwananchi Insurance,” alisema.
 
Aliongeza kusema kwamba, mshtakiwa alikuwa amewaajiri wanawake wawili kwa ajili ya utoaji wa huduma hizo za bima kwa kampuni hewa iliyojulikana kwa jina la Imock.
Wakili wa serikali Alex Mwita alisema mahakama iangalie namna ya kumpunguzia adhabu mshtakiwa kwa kuwa hajawahi kutenda kosa lolote.
 
Hakimu alitoa fursa kwa mshtakiwa kujitetea ambapo alisema kwamba hilo ni kosa lake la kwanza na kwamba ana watu wanaomtegemea, hivyo mahakama iangalie namna ya kumpunguzia adhabu.
 
“Naomba mahakama inipunguzie adhabu kuwa nina watoto wawili wa marehemu kaka yangu ninaowasomesha chuo kikuu cha RUCO, lakini watoto wangu mwenyewe wananitegemea na pia mama yangu ni mtu mzima ananitegemea mimi,” alisema.
Aidha, alisema pia anafanya kazi za kijamii kupitia shirika lisilo la kiserikali la Iringa Youth Development Association (IYODEA).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni